Kocha mkuu wa Toto Africans Fulgence Novatus amesema kikosi chake kina nafasi nzuri ya kufanya kweli kwenye mechi yao ijayo dhidi ya Simba kwa sababu watakuwa wakicheza kwenye uwanja wao wa nyumbani CCM Kirumba Mwanza.
Novatus amesema watakuwa katika nafasi nzuri ya kupata matokeo kwa sababu wanajiandaa kwa ajili ya mchezo huo lakini kikubwa kwao ni kuwa kwenye uwanja wa nyumbani.
“Mechi ijayo tunacheza na Simba, sisi tunajiandaa na yoyote kadiri tunavyoweza, lakini kwakuwa tutakuwa nyumbani tunachoamini sisi tutakuwa katika nafasi ya kufanya vizuri kwa sababu bado tuna nafasi ya kufanya hivyo,” alisema Novatus wakati akizungumza na Shekhan Mzaina mara baada ya mechi yao ya ugenini dhidi ya Majimaji FC kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Novatus ambaye kikosi chake kilipoteza mchezo dhidi ya Majimaji kwa kuchapwa 4-0 alisema: “Matatizo yalijitokeza ndani ya mchezo na tulikuwa tunapungukiwa uwezo wa kukaba lakini pia mazingira ya uwanja yamechangia kidogo sisi kushindwa kufanya vizuri.”
Toto Africans inatarajia kuikabili Simba April 12, 2017 kwenye uwanja wa CCM Kirumba huku timu hizo zikiwa na malengo tofauti. Simba inapambana kuhakikisha inafanya vizuri kwa kushinda mechi zake zilizosalia ili kujiwekea mazingira ya kushinda ubingwa wa VPL wakati Toto Africans wenye wanataka kujinasua wasishuke daraja.
Simba ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara ikiwa na pointi 55 baada ya kucheza mechi 25 huku Toto Africans wao wakiwa nafasi ya 14 kwa pointi zao 23 baada ya mechi 25.
Kakita kipindi cha misimu ya hivi karibuni, Simba wamekuwa wakipata upinzani mkubwa kutoka kwa Toto japo wana kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi yao ya mzunguko wa kwanza msimu huu kwa magoli 3-0 kwenye uwanja wa Uhuru, Dar.
Source:shaffihdauda
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment