Monday, April 24, 2017

Bodi 10 vyama vya korosho zavunjwa kwa ubadhirifu

SERIKALI kupitia Mrajisi wa Vyama vya Ushirika imeanza kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu wa fedha na mali za vyama hivyo nchini baada ya kuvunja bodi 10 za vyama hivyo vya wakulima wa korosho wilayani Nachingwea mkoani Lindi. 
Aidha, makatibu wakuu 10 wa vyama hivyo wameondolewa madarakani na bodi mpya za muda zimewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika. Kaimu Mrajisi Msaidizi, Revocatus Nyagilo ambaye aliongoza vikao vya kuvunjwa bodi hizo kwa niaba ya mrajisi wilayani Nachingwea, alisema hatua hiyo inatokana na uchunguzi uliofanywa na Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC) kwa kushirikiana na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO).
Nyagilo alisema uchunguzi huo uliofanyika mwaka jana, ulibaini ubadhirifu wa mabilioni ya fedha na mali katika vyama hivyo katika mikoa ya Lindi na Mtwara na hivyo kuamua kuitisha mikutano maalum ya vyama hivyo katika mikoa hiyo kwa hatua zaidi. Akiendesha mikutano hiyo kwa niaba ya Mrajis mwishoni mwa wiki, alisimamia kuvunjwa kwa bodi hizo na kuondolewa madarakani makatibu wakuu wa vyama hivyo 10 kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Namba 6 ya Mwaka 2013 na Kanuni zake za mwaka 2015.
Katika taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi hiyo wilayani Nachingwe ilieleza kuwa vyama ambavyo bodi zake zimeondolewa madarakani na makatibu kuvuliwa nafasi zao Aprili 20 mwaka huu kwa ubadhirifu ni Ndomondo, Naipanga, Chiumbati, New Stesheni na Mchonda.
Vingine ni Makina, Mkotokuyana, Nache, Namikango na Ndangalimbo. Vyote 10 ni Vyama vya Ushirika vya Mazao na Masoko (AMCOS) na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.
Nyagilo alisema katika mikutano hiyo maalum mbali na kuvunjwa bodi na kuondolewa madarakani makatibu wakuu, bodi mpya za muda zimewekwa. “Hakukuwa na changamoto iliyojitokeza zaidi ya uelewa mdogo wa Sheria ya Vyama vya Ushirika miongoni mwa wanachama, viongozi pamoja na watendaji wao,” alisema.
Ofisa Habari wa TCDC, Ntambi Bunyazu, akizungumza na gazeti hili jana alisema mikutano hiyo inafanyika katika mikoa miwili; Mtwara na Lindi na itahusisha vyama vya ushirika wa mazao ambavyo viongozi wake wameonesha kutokufanya vizuri katika uendeshaji wa vyama hivyo.
“Hili linalofanyika ni endelevu,” alisema Bunyazu na kufafanua kuwa uchunguzi na ukaguzi kwa vyama hivyo ulifanyika mwaka mwaka. Taarifa kutoka katika tovuti ya TCDC ya www.ushirika.go.tz, ya Machi 24 mwaka huu, yenye kichwa cha habari kisemacho “Wabadhirifu katika Vyama vya Ushirika, Wadhibitiwe” imeeleza kuwa, Serikali kupitia (COASCO) ilifanya ukaguzi wa hesabu za AMCOS zilizopo katika wilaya za mkoa wa Mtwara kwa msimu wa mwaka 2015/2016 ulioishia tarehe 30 Aprili, 2016.
“Ukaguzi huo ulifanyika kutokana na malalamiko yaliyotolewa na wakulima ya kufanyika kwa ubadhirifu katika AMCOS ambazo wao ni wanachama. Taarifa ya COASCO ilionesha matatizo mbalimbali ya kiutendaji, usimamizi na ubadhirifu katika AMCOS za mkoani Mtwara.
Matatizo yaliyojitokeza yalitakiwa kufanyiwa kazi na Mrajis wa Vyama vya Ushirika kwa mujibu wa Sheria....,” ilieleza taarifa hiyo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ili kufanikisha kazi ya kushughulikia matatizo ya vyama vya ushirika mkoani Mtwara, hasa AMCOS, TCDC ilizikutanisha mamlaka za Kiserikali kwa maana ya Serikali katika ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri za mkoa wa Mtwara, wabunge, COASCO, Bodi ya Korosho TCDC kufanya kikao cha pamoja.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa lengo la kikao hicho ni kujadili matokeo ya taarifa ya ukaguzi wa AMCOS. “Mrajisi wa Vyama vya Ushirika alitumia kikao hicho kuweka wazi hatua anazokusudia kuzichukua kwa wahusika wote wa ubadhirifu katika vyama hivyo”. Hatua ambayo ilifikiwa pia kwa mkoa wa Lindi.

source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment