Tuesday, March 21, 2017

Timu ya Nape kuanika ukweli wa Clouds leo

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye (pichani) ameunda timu ya watu watano wafanye kazi kwa saa 24 kuanzia jana, wakutane na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kujua undani wa kilichotokea Ijumaa iliyopita usiku saa 5:30 kwa kuvamia kituo cha Habari cha Clouds Media akiwa na askari wenye silaha.
Akizungumza Dar es Salaam jana baada ya kutembelea Clouds Media Group, Mikocheni, Nape alisema kama serikali, kilichotokea ni kitendo ambacho kimewashtua wengi na hata dunia kwa ujumla kwa kuwa hata katika historia haijawahi kutokea suala kama hilo.
Alisema kutokana na kilichotokea, ameunda timu ya watu watano wakifanya kazi kwa saa 24 ili kujua na upande wa pili ambao ni wa Makonda unazungumziaje suala hilo na baadaye watamkabidhi ripoti ambayo ataitoa leo saa 8:00 mchana.
Aliwataja wanaounda timu hiyo itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Abbas Hassan, ni Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi, Mhariri Mwandamizi kutoka Kampuni ya The Guardian, Jesse Kwayu, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamhuri na Mhariri wa Wapo Radio, Neng’ida Johannes.
Waziri Nape alisema serikali imesikitishwa na jambo hilo, lakini lazima kutenda haki kwa kumsikiliza pia mkuu wa mkoa na watu wake ili kujiridhisha halafu ndipo hatua nyingine zitakapoweza kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba alisema Spika wa Bunge ameiomba kamati hiyo kufika na kujua kilichotokea, na kimsingi kilichofanywa na mkuu huyo wa mkoa.
Alisema kamati inasubiri ripoti ya serikali, ndipo itashauri hatua za kuchukuliwa na kwamba wana jukumu kubwa la kulinda waandishi wa habari na kamwe haikubaliki kwa mtu mmoja mwenye silaha kuweza kutumia madaraka namna hiyo kwani siku nyingine anaweza kuyatumia katika migahawa au nyumbani kwa watu.
Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Reginald Mengi alisema hawezi kutoa lawama kwa yeyote hadi hapo matokeo yatakapotolewa, lakini akaongeza kuwa kilichotokea ni aibu kwa Taifa, kwa kuwa haijawahi kuzoeleka na vyombo vya habari vinalaani kwa nguvu zote na tasnia hiyo itatumia nguvu zake zote kulinda uhuru wake, sio kwa bunduki ila kwa njia ya kiungwana.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alilezea namna Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alivyovamia ofisi za chombo hicho cha habari akiambatana na askari waliobeba silaha.
Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi kinachorushwa na kampuni hiyo jana, Mutahaba alisema kwa niaba ya kampuni hiyo, wanalaani kitendo hicho cha Makonda kwa kuwa kimewaacha katika hali mbaya wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema chanzo cha tukio hilo, kilianza tangu Alhamisi iliyopita wakati uongozi wa kampuni hiyo ulipokuwa kwenye kikao na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRA), ambapo walipata ugeni wa RC Makonda katika kikao hicho.
“Baada ya hapo wakati kikao kimemalizika nikiwa natoka nikakutana na vijana wanatangaza katika kipindi cha Shirika la Wambea Duniani (SHILAWADU) kupitia kampuni hiyo, wakiwa wanazungumza na mkuu huyo wa mkoa,” alisema Mutahaba.
Alisema mmoja wa vijana wale alimfuata na kumueleza juu ya kuwepo kwa fununu za habari kubwa inayomhusu Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kuzaa na mmoja wa waumini wake, lakini bado fununu hizo pamoja na kukamilika upande mmoja, hazijathibitishwa upande wa pili.
“Niliwaambia kuwa kama habari hiyo hata kama ni nzuri vipi kama bado haina upande wa pili kama maadili ya taaluma ya uandishi wa habari yanavyotaka kamwe isirushwe hewani. Sikuishia hapo nilimpigia simu mkuu wa vipindi Carry, nikamuonya asiruhusu habari hiyo iruke hewani kama haijawa balanced,” alifafanua.
Alisema siku hiyo, majira ya saa 10 jioni alipigiwa simu na Askofu Gwajima akiulizia taarifa za kuwepo kwa habari inayomhusu inayotarajiwa kurushwa katika vyombo vya habari vya kampuni hiyo kupitia kipindi cha SHILAWADU.
Alisema alimjibu mtumishi huyo wa Mungu kuwa ni kweli alikuwa na taarifa za kuwepo kwa habari hiyo, ingawa yeye mwenyewe haifahamu kiundani na kufafanua kuwa alishaagiza isirushwe hewani mpaka itakapokamilika kwa upande wa pili kupatikana.
“Hata hivyo, nimueleza kuwa habari ile si CMG pekee ndio walikuwa nayo bali kulikuwa na vyombo vingine vya habari, hivyo si jukumu la Clouds kuzuia vyombo vingine ama viitoe au visiitoe,” alisema.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment