Monday, February 20, 2017

Siri yafichuka wanawake wengi kujifungua kwa upasuaji

WANAWAKE wengi kwa sasa wanajifungua kwa njia ya upasuaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mfumo wa maisha, vyakula, mwili kukosa mazoezi huku baadhi wakiomba wenyewe kufanyiwa upasuaji, imefahamika.
Aidha, imeelezwa kuwa baadhi ya hospitali zinalazimisha upasuaji kama njia ya kutafuta fedha, jambo lililoelezwa kuwa ni kinyume cha maadili ya tiba nchini.
Gazeti hili limezungumza na madaktari mbalimbali, wakiwemo madaktari bingwa wa wanawake na wanajamii kwa ujumla kuhusu sababu mbalimbali zinazohusishwa na hali halisi ya uzazi wa wanawake kwa sasa.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Dk Erasto Rite alisema njia ya upasuaji kwa mjamzito inayotumika kuzalisha mtoto mmoja au zaidi (caesarean section), hutumika kipindi ambacho uhai wa afya ya mama na mtoto upo hatarini.
Alisema takwimu zinaonesha kwamba ongezeko kubwa la njia ya upasuaji kwa wajawazito ambapo ni kati ya asilimia 16.4 mpaka 28 ya akinamama wanaojifungua, huku idadi ikiwa juu kwa kina mama wanaoishi mijini ikilinganishwa na wanaoishi vijijini.
Dk Rite alisema hiyo inachangiwa na kubeba ujauzito katika umri mkubwa, kukua kwa teknolojia na baadhi ya kina mama wenyewe kuchagua njia hiyo.
Alisema kwa upande wa kina mama wanaoishi vijijini, njia hiyo imeanza kuongezeka kutokana na baadhi yao kutumia dawa za kienyeji za kuongeza uchungu (dawa za wepesi), ambazo husababisha wengi kuishia kufanyiwa upasuaji.
Alisema hiyo pia huchangiwa na dawa hiyo kutolewa bila vipimo na pia wengi wanatumia dawa hizo wakati hakustahili kupewa na hivyo kumsababisha kupata uchungu mkali unaohatarisha maisha yake na kulazimika kupasuliwa.
Kwa upande wake, daktari wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Regency Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema hali hiyo huchangiwa na mfumo wa mabadiliko ya maisha kipindi cha nyuma na ilivyo sasa.
Alisema zamani wanawake walikuwa wakila vyakula vya asili na kufanya shughuli mbalimbali ambazo zilikuwa kama mazoezi ya kumsaidia kuuweka mwili sawa, lakini kwa sasa ni tofauti, wanawake wengi hula vyakula ambavyo havina mpangilio maalumu na hawajishughulishi kuweka mwili sawa.
Aidha, alisema sababu nyingine inayochangia wanawake kufanyiwa upasuaji ni shinikizo la damu au mtoto kukaa vibaya au mtoto kuwa mkubwa na hivyo kushindwa kutoka kwa njia ya kawaida.
Alisema hiyo ndiyo hasa dharura inayotakiwa kuzingatiwa mjamzito kufanyiwa upasuaji na si vinginevyo. Mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, Juliana Joseph ambaye amejifungua watoto wawili kwa njia ya upasuaji, alisema alitamani kujifungua kwa njia ya kawaida, ila tatizo kubwa linalomsumbua wakati akiwa mjamzito ni shinikizo la damu na hivyo madaktari humshauri kwamba ili kuokoa maisha yake na ya mtoto ni lazima kufanyiwa upasuaji.
“Wakati nikiwa hospitali moja ya binafsi nilipokuwa najifungua mtoto wangu wa kwanza, alitokea mama mmoja akiwa ameshapata uchungu, madaktari walimshauri hawezi kujifungua kawaida kwa kuwa mtoto ni mkubwa ila walibishana sasa mama yule alikataa upasuaji akalazimisha kusukuma mtoto.
“Kutokana na hali kuwa mbaya na mtoto kukaa njiani muda mrefu, mtoto alizaliwa amechoka sana na baada ya kuzaliwa alikaa kwenye mashine ya kupumulia siku mbili na ya tatu akafariki, hivyo niliamini kwamba mama yule alichangia kumuua mwanawe, hivyo tunaposhauriwa na madaktari tukubali na tusibishane nao kwa kuwa siamini kama inawezekana mtu mwenye uwezo wa kujifungua kawaida ukalazimishiwa upasuaji, hiyo ni imani potofu,” alisema Juliana.
Naye Amini Salum alisema amejifungua mtoto kwa njia ya upasuaji na hiyo imesababishwa na mtoto wake kukaa vibaya na hivyo kushindwa kutoka kwa njia ya kawaida.
Kwa upande wake, mganga wa wanawake katika Hospitali ya Tumbi wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani ambaye hakuwa tayari kutaja jina gazetini, alisema upasuaji unapaswa kufanyika pale inapotokea tatizo kwa mjamzito na si kitu kinachopendwa na madaktari kumfanyia mtu.
Hata hivyo, alisema zipo taarifa kuwa, baadhi ya wanawake huomba kufanyiwa upasuaji hasa katika hospitali binafsi kwa kile kinachodaiwa hawataki kuharibu maumbile yao ya uzazi.
“Sijui nani aliwaambia maumbile yanaharibiwa kwa kuzaa kwa njia ya asili.
Huo ni utaratibu aliyouweka Mungu mwenyewe hata vitabu vitakatifu vinaeleza.
Uke huwa kama mpira na hutanuka wakati wa kujifungua na baada ya muda mfupi, hurejea katika hali yake, sasa hii dhana potofu sijui wameitoa wapi,” alisema daktari huyo.
Kuhusu hospitali binafsi, alisema wapo wanaowashauri wajawazito kufanyiwa upasuaji kwa tamaa za fedha, jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya kazi yao na kuwataka kuzingatia maadili na kufanya upasuaji inapobidi lakini kama mjamzito hana tatizo lolote la dharura linalohitaji upasuaji, aachwe ajifungue kawaida.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam, Dk Munawar Kaguta alisema wanawake wengi wa mjini wanaomba wenyewe madaktari kuwazalisha kwa upasuaji.
Dk Kaguta alisema hayo hivi karibuni katika mahojiano na gazeti hili kuhusu masuala ya uzazi.
Alifafanua kuwa wanawake wa mjini wanadanganywa na taarifa mbalimbali wanazozipata katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ambazo zinaonesha kuwa kujifungua kwa kawaida ni hatari.
“Hawa wanawake wa mjini wanadanganywa na mitandao ambayo wanaingia kutafuta taarifa za uzazi, mwisho wa siku wakija hospitali wanaomba wao wenyewe kufanyiwa upasuaji kutoa mtoto,” alisema Dk Kaguta.
Daktari huyo alisema mbali na taarifa za mitandaoni, pia wanashawishiana na kupeana taarifa nyingine zisizo sahihi, wakielezana athari nyingi zinazoweza kumpata mama anapojifungua kawaida, ikiwa ni pamoja na kupata uchungu mkali wakati wa kujifungua.
Alisema pamoja na sababu zote hizo madaktari wengi huwazungusha na wanapolazimisha sana wakienda hospitali kwa ajili ya kujifungua mwisho wanajifungua wenyewe kwa njia ya kawaida.
Dk Kaguta alisema kila jambo lina madhara yake, alisema mwanamke kupata uchungu wakati wa kujifungua ni kawaida na kwamba hapa nchini hakuna wataalamu wa kutosha kwa ajili ya dawa za kupunguza uchungu.
“Dawa zipo lakini tatizo wataalamu wa kuzichoma, zina utaalamu wake na ambao kwa hapa nchini sio wengi,” alisema Dk Kaguta na kuongeza kuwa wataalamu hao wakipatikana wa kutosha na dawa zifike mpaka katika hospitali za serikali itasaidia kupunguza idadi ya wanaojifungua kwa upasuaji.


0 comments:

Post a Comment