Thursday, January 19, 2017

Kaimu Jaji Mkuu aahidi haki kwa haraka na uwazi

KAIMU Jaji Mkuu mpya wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameahidi kuweka mkazo katika matumizi ya Tehama katika kuendesha kazi za Mahakama kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka.

Jaji Juma alitoa ahadi hiyo baada ya kuapishwa, tukio lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Jaji Juma awali alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na atashika nafasi hiyo mpaka hapo Rais Magufuli atakapofanya uteuzi wa Jaji Mkuu.
“Katika kuwahudumia wananchi katika kutoa haki na kwa haraka tutatumia teknolojia ya habari ili haki iweze kupatikana haraka kuliko sasa,” alisema Jaji Juma.
Alisema alipata nafasi ya kusoma sera ya Tehama iliyotolewa Mei mwaka jana ambayo inatoa picha ya nchi miaka 20 ijayo kuonesha nchi inatakiwa kwenda wapi ambapo na mahakama inatakiwa kutekeleza.
“Mpango wangu ni kwamba, kesi zinasajiliwa katika mtindo huo ili kuhakikisha haki inapatikana haraka na kwa uwazi zaidi ya ilivyo sasa,” alisema Jaji Juma na kuwapongeza majaji wakuu waliomtangulia ambao waliweka msingi wa mabadiliko katika mahakama ikiwa ni pamoja na kuweka mpango mkakati unaosaidia katika utendaji kazi.
“Sheria nyingi zimebadilika, fedha nyingi zimepatikana na vilevile mpango mkakati wa mahakama, sasa ni kuutekeleza mpango huo ….. wao wameshamaliza kazi yao sasa ni kupunguza maneno”, alisema Jaji Juma.
Aidha alimshukuru pia Rais John Magufuli kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo ili aweze kuwahudumia wananchi katika kutoa haki. Rais Magufuli juzi alimteua Jaji Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania kuchukua nafasi ya Jaji Mohamed Chande Othman ambaye amestaafu.
Katika tukio hilo, Jaji Mkuu mstaafu alisema katika mambo ambayo hata yasahau katika kazi zake ni pamoja na kubadilisha watumishi wa mahakama kutambua kuwa ni chombo ambacho kinawajibika kwa wananchi.
“Hili ni jambo ambalo lipo na linaendelea katika kuhakikisha kwamba mahakama ni chombo ambacho kinatoa haki na pia kwa wakati kwa Watanzania wote,” alisema Othman na kuongeza kuwa Mahakama iko kwenye kasi ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inaitaka na kuwataka watendaji wanaobaki kuongeza kasi hiyo.

Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video



0 comments:

Post a Comment