MKAZI wa Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa, Richard Mwananzila anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kujimilikisha Ziwa Sundu lililopo katika Kata ya Sundu Wilaya ya Kalambo, huku akiwatisha wavuvi kuwa yeye ni mtoto wa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba.
Amri ya kukamatwa kwake ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura, ambaye alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD) kumsaka mtu huyo kwa udi na uvumba na kumfikisha mahakamani.
Mbali ya kujimilikisha Ziwa, Mwananzila anashutumiwa pia kwa kuuza zana haramu za uvuvi na kuwatapeli wavuvi fedha zao.
Mkuu huyo wa wilaya alisema mtu huyo huwatishia wavuvi wanaovua katika ziwa hilo kutovua bila kumpa fedha kwa vile ziwa hilo ni mali yake na kuwataka pia kununua zana haramu za uvuvi kutoka kwake na wanaogoma huwazuia akisema yeye ni mmiliki halali wa ziwa hilo.
“Kama vile haitoshi nimeelezwa pia kuwa mtu huyu anajigamba kuwa hakuna kiongozi yoyote wa serikali mwenye ubavu wa kumkamata kwa kuwa yeye ni mtoto wa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Pamoja na kuagiza kukamatwa kwake haraka, Binyura pia alitoa amri ya kuteketezwa kwa zana haramu za uvuvi za mfanyabiashara huyo zilizokakamatwa kufuatia doria maalumu zilizofanyika katika ziwa hilo na zile zilizokamatwa katika Kijiji cha Kasanga kilichopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo.
Aidha aliwaagiza askari wa kikosi cha doria kuendelea kuwasaka wavuvi wengine wanaotumia zana haramu za uvuvi na kuteketeza raslimali zinazopatikana katika Ziwa Sundu na Ziwa Tanganyika yaliyopo wilayani humo kwa kufanya doria za mara kwa mara na za kushtukiza.
“Nakuagiza OCD wa Kalambo hakikisha mfanyabiashara huyu (Mwananzila) atatafutwa popote pale alipo mkamateni ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria iweze kuchukua mkondo wake. “Isitoshe nawaagiza askari wa kikosi cha doria muendelee kuwasaka wavuvi wanaotumia zana haramu za uvuvi kwa kufanya doria za mara kwa mara na za kushtukiza ili kuzilinda raslimali zilizopo katika Ziwa Sundu na Ziwa Tanganyika,“ aliaagiza.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutoandikwa gazetini kutokana na kumuhofia Mwananzila, baadhi ya wavuvi walidai wanamfahamu mfanyabiashara huyo kuwa ni mkazi wa Sumbawanga mjini.
“Huyu mfanyabiashara anaitwa Richard Mwananzila ni mkazi wa mjini Sumbawanga amekuwa akitutishia sisi wavuvi wageni tunaomiliki leseni za uvuvi kwamba tusiponunua zana haramu za uvuvi kutoka kwake basi hataturuhusu kuvua samaki katika Ziwa lake la Sundu kwa kuwa ana hati miliki yote ya ziwa hilo huku akitishia kuwa yeyote atakayemfuatilia atakiona cha moto kwa kuwa ni mtoto wa Waziri Dk Tizeba,” alisema mmoja wa wakazi hao akiwa na hofu kubwa ya kugunduliwa.
Source:habarileo
0 comments:
Post a Comment