Monday, November 21, 2016

‘Tozo kuvusha magari daraja la Nyerere iangaliwe upya’

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, amelitaka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuangalia upya tozo ya magari kuvuka katika daraja la Nyerere wilayani humo, ikiwa ni pamoja na kutaka magari yote ya serikali na watumishi wa umma wanaofanya kazi katika halmashauri hiyo kutolipa tozo hiyo.
Alisema kitendo cha magari ya halmashauri hiyo na watumishi wa umma wanaoishi nje ya halmashauri kutozwa fedha kuvuka katika daraja hilo kinaleta changamoto kubwa na kukwamisha ufanisi.

Mgandilwa alitoa ombi hilo jana wakati wa ziara ya siku mbili ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyoifanya katika wilaya hiyo. Alimuomba mkuu huyo wa mkoa kuingilia kati suala la gharama hizo na kuitaka NSSF kuziondoa kwa magari yote ya halmashauri na watumishi.
“Kila gari ya halmashauri inayopita katika daraja hili inatozwa fedha. Hasa ikizingatiwa kuwa halmashauri hii ni mpya hivyo watumishi wengi wanatokea nje ya halmashauri,” alisema Mgandilwa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala la tozo ya daraja hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyrara, alikiri kupokea malalamiko ya watu wengi kutaka kupunguziwa au kuondolewa tozo hiyo.
“Ni kweli tumekuwa tukipokea malalamiko hayo kutoka kwa wananchi mbalimbali, lakini suala ni kwamba sisi kama NSSF huwa hatupangi viwango vya tozo za kuvuka daraja bali tunapokea maelekezo kutoka wizara husika (Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi),” alisema Kahyarara.
Alisema atawasilisha suala hilo katika wizara husika ili kuona uwezekano wa kuondoa tozo hiyo ama kupunguza. Mbali na hayo, Kahyarara alitaja changamoto zingine kuwa ni vijana kuligeuza daraja hilo kuwa kijiwe na wengine kuwa na nia ovu ya kulihujumu kwa kuharibu miundombinu, ingawa ulinzi umeendelea kuimarishwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Makonda, alisema chanzo cha magari ya halmashauri hiyo kutozwa tozo ni kutokana na mchakato na ujenzi wa daraja hilo kufanyika kabla ya halmashauri ya manispaa ya Kigamboni kuanzishwa.
“Hivyo hawakufikiria kama kutakuwa na muingiliano huu. Hivyo tutajitahidi kulipatia ufumbuzi kwa kuzungumza na mamlaka husika,” alisema Makonda.



Source:habarileo

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video





0 comments:

Post a Comment