Sunday, November 20, 2016

Makonda aagiza watumishi watoke ofisini


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka watumishi katika halmashauri za mkoa huo kufanya kazi kwa kujituma na kuacha kukaa maofisini kusubiri mishahara.
Makonda ametoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 10 katika mkoa huo iliyoanza jana katika wilaya hiyo.
Amesema asilimia 80 ya watumishi hao hawapendi kufanya kazi kwa kujituma jambo linalosababisha wananchi kukosa huduma stahiki.
"Wakuu wa idara hawapendi kutoka ofisini, wengi wao wakidai hakuna bajeti. Watumishi hawana morali kabisa wa kufanya kazi wengine wanashindwa kabisa hata kubuni mbinu za kupata fedha nje ya bajeti. Kuna wadau wengi wanaoweza kutusaidia changamkeni," amesema Makonda.
Aidha aliwataka maofisa biashara kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabiashara na kuwa washauri na namna ya kujenga biashara zao jambo ambalo litaleta hamasa ya ulipaji kodi kwa wafanyabiashara hao.
"Maofisa biashara wengi ni mizigo hawana uhusiano mzuri na wafanyabiashara, wengine hata hawawafahamu zaidi ya kuwapa leseni, sitaki muishie kwenye leseni pekee jengeni uhusiano na watu hawa mtawapa hamasa hata kwenye ulipaji kodi," amesema.
Pia amewataka watumishi hao kuepuka kushiriki vitendo vya rushwa wakati wa ulipaji wa fidia badala yake wafanye kazi kwa haki na usawa lengo likiwa ni kuleta maendeleo katika wilaya hiyo.
"Miradi mingi ya fidia watendaji wamekula acheni kabisa dhambi hii geukeni kuwa msaada kwa wananchi wanaowaamini," alisisitiza. Katika hatua nyingine Makonda amepiga marufuku uchimbaji kokoto katika eneo la Mjimwema na kuitaka halmashauri hiyo kutafuta namna ya kutumia maeneo hayo ili yasitumike kama mapango ya kihalifu.
"Nakupongeza kwa hatua ulizochukua Mkuu wa Wilaya za kuzuia uchimbaji huu usirudishwe nyuma na wachimbaji hawa, tafuteni namna haya yasibaki kuwa mahandaki ya kujificha wahalifu," amesema.
Makonda alisema uchimbaji huo umesababisha uharibifu wa nyumba nyingi ambazo zimebaki zikining'inia na kuwa hatari kwa wakazi wa nyumba hizo.

Source:habarileo

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video



0 comments:

Post a Comment