Sunday, November 20, 2016

Majaliwa atoa siku 18 umeme ufike kiwandani


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku 18 kwa mkandarasi wa umeme kwenye kiwanda cha Kiluwa Steel Group awe amemaliza kazi ya kuweka umeme mkubwa ili kiwanda hicho kianze kazi.
Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Pwani waliofika kiwandani hapo eneo la Mlandizi wakati akikagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Julai 12, mwaka huu alipozuru kiwanda kwa mara ya kwanza.

"Nilipokuwa hapa mara ya kwanza niliagiza itengenezwe njia ya reli kutoka njia panda ya reli ya kati, lakini pia niliagiza uwekwe umeme wa msongo mkubwa ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji mapema mwakani. Nimefarijika kukuta maagizo haya yametekelezwa kwa kiasi kikubwa isipokuwa hili la umeme.
"Mkandarasi ameomba siku 14, nimempa hadi tarehe 7 Desemba ahakikishe umeme unafanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Sasa hivi wameanza test lakini itachukua muda ili transfoma iweze kuhimili mzigo mkubwa... hili ni suala la kitaalamu kwa hiyo tuwape muda."
Waziri Mkuu pia alisema amefarijika kusikia kuwa orodha ya watu wanaodai fidia sababu ya kupisha njia ya reli ijengwe, imeshawasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na mwenye kiwanda yuko tayari kuwalipa mara taratibu zitakapokamilika.
Akiwasilisha taarifa fupi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema haelewi ni kwa nini mkandarasi huyo anazidi kuomba siku 14 ili kukamilisha wakati aliahidi kuwa siku 14 za awali zingetosha kukamilisha kazi hiyo.
Kuhusu fidia kwa wananchi na halmashauri ya wilaya hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wananchi waliopisha njia wanadai fidia ya Sh milioni 95.76 na halmashauri inadai Sh milioni 307.26 na kwamba jumla yote ni Sh milioni 403.
Alipotakiwa ajieleze mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Dekan Group Ltd, Desderius Luhaga ambaye amepewa kazi ya kuweka umeme na transfoma Mlandizi alisema anahitaji siku 14 ili aweze kukamilisha kazi hiyo.
"Kazi kubwa ya umeme tumeshaifanya na hii ni ya umeme wa msongo wa kilovoti 132, na tumeanza kutesti umeme katika baadhi ya mitambo hapa kiwandani, lakini tunahitaji siku karibu tano ili transfoma ipoe tangu tulipoifunga ndipo iweze kupokea mzigo mkubwa. Kisha tutaanza kuunganisha katika maeneo mengine madogo madogo humu ndani," alisema.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Masanja Kadogosa alisema shirika hilo limetumia Sh milioni 863 kukamilisha ujenzi wa reli ya kilometa 5 kutoka njia panda hadi kwenye kiwanda hicho ambapo kati ya hizo kilometa 1.5 zimo ndani ya kiwanda.
Alisema hadi sasa wameshaweka njia nne za reli, moja ikiwa ni mahususi kwa ajili ya kubeba makaa ya mawe.
"Tulilazimika pia kujenga kalavati katika eneo moja kwa sababu palikuwa na shimo kubwa. Tumetumia fedha kidogo kwa sababu tumetumia mafundi wetu badala ya makandarasi," aliongeza.

Source:habarileo

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video




0 comments:

Post a Comment