Thursday, October 20, 2016

WAFANYABIASHARA ARUSHA WAMPA BIG UP JPM

WAFANYABIASHARA wakubwa wa Mkoa wa Arusha wamepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais John Magufuli katika mwaka wake mmoja madarakani, ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kudhibiti matumizi ya fedha ya umma na kurejesha uadilifu na uwajibikaji katika kazi.

Waliyasema hayo jana katika mkutano na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo mjini hapa.

Alikutana nao kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.

Mfanyabiashara Nicholaus Duhia, alisema Rais Magufuli amesimamia vema ulipaji kodi, kurudisha heshima ya uadilifu serikalini na kupiga vita ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma zilizokuwa zikitumika kiholela bila ya kuwa na utaratibu maalumu.

Duhia ambaye ni wakili, mkaguzi wa hesabu na ushauri wa kodi wa kampuni ya Tax Plan Associates ya Arusha, alisema hakuna anayeweza kubisha kuwa Rais Magufuli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Alisema na kutoa ombi kupitia kwa Gambo kuwa Rais Magufuli katika mwaka wa pili wa uongozi wake anapaswa kurudisha imani na amani kwa wafanyabiashara nchini ili wafanye kazi bila woga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa A Lodhia Group Enterprises, Sailesh Pandit, alisema mbali ya kumkubali Rais Magufuli kwa utendaji kazi wake wa falsafa ya Hapa Kazi Tu, amesema anakunwa pia kwa jinsi heshima ya kazi ilivyorejea serikalini, huku watendaji wa serikali wakichapa kazi kwa weledi.

Wafanyabiashara Willibrod Chambulu wa Kibo Safaris na Atul Nittal wa Mount Meru Millers wameiomba serikali iangalie namna ya kupunguza utitiri wa kodi. Gambo aliwahakikishia kuwa serikali itakuwa imara na kuwalinda na kuwasaidia watakapokwama, lengo likiwa kuwataka wafanye kazi kwa ufanisi, bila ya kipingamizi.


Source: mtembezi

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video





0 comments:

Post a Comment