Ikiwa ni miezi mitatu tangu Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji ‘MO’ kuahidi kutumia nusu ya utajiri wake kusaidia watu wenye uhitaji duniani, amezungungumza kwa mara ya kwanza ni sehemu gani ambapo watu wake watanufaika zaidi na pesa hizo.
Akizungumza na wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali nchini, MO Dewji amesema kuwa pamoja na kuahidi kusaidia watu wenye uhitaji duniani kwa nusu ya utajiri wake, lakini sehemu kubwa ya pesa hizo itatumika kuwanufaisha watanzania.
Dewji amesema kuwa anafahamu kwa kiasi kikubwa changamoto ambazo zinawakabili wananchi wa taifa lake lakini kupitia ahadi ambayo aliitoa kupitia kundi la The Giving Pledge atahakikisha watanzania wanafaidikana utajiri wake.
“Nimezaliwa Tanzania na nitakufa Tanzania kwahiyo ni muhimu sana na huwa watu wananiuliza umepledge ukiwa mdogo sana, unajua maisha hatujui kama tutaishi kwa asilimia 100 kwa hiyo tunatakiwa kurudisha kwa Mungu, jamii, na kwa nchi kwa kutoa msaada na unajisikia vizuri kama binadamu kufanya hivyo,” amesema Dewji.
Aidha Dewji amesema kwasasa amekuwa akitoa misaada kwa jamii kupitia Taasisi yake ya MO Dewji ambayo imekuwa ikiwapa msaada watu wa makundi mbalimbali ikiwepo kuwapa wafanyabiashara mikopo siyo na riba.
“Sasa nina taasisi yangu na mambo mengi nafanya kupitia taasisi hiyo, tunadhamini wanafunzi wasio na uwezo wapate kusoma, tunasaidia huduma za kiafya kwa jamii, tunawapa wajasiliamali mikopo isiyo na riba hii yote ni kuona nasaidia sehemu ya jamii inayonizunguka na wengine waweze kufaidika na uwepo wangu,” alisema Dewji.
Awali akielezea lengo la kongamano, Mratibu wa kongamano hilo, John Muruga amesema wameandaa kongamano hilo ili kuwakutanisha wahitimu wa vyuo vikuu ambao wana nia ya kujiajiri ili waweze kupata ushauri wa njia gani wanaweza kuzitumia na kufikia malengo ambayo wamejiwekea.
“Wapo wahitimu wengi ambao wanamaliza kila mwaka na serikali haina ajira za kutosha kuwaajiri wahitimu wote na sehemu kubwa ya watu ambao wanawaajiri watu hawa ni sekta binafsi lakini wengine wanataka kujiari wenyewe na hapa tumewashirikisha wale tu ambao wanataka kujiajiri,
“Ujio wa mtu kama Dewji ni muhimu kwa sababu ameshafanikiwa katika sekta ya ujasiriamali kwahiyo imani yetu ni kuwa wahitimu hawa watapata kitu cha kujifunza kipya ambacho kinaweza kuwasaidia wao kama watu ambao wanandoto ya kufanikiwa kama Dewji,” alisema Muruga.
Source:dewjiblog
0 comments:
Post a Comment