Thursday, October 6, 2016

Mkuu wa Magereza Dodoma kuchunguzwa

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza mkuu wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, kuchunguza sababu ya mkuu wa magereza mkoa huo, Antonino Kilumbi,kwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi badala ya karakana ya magereza.


Magereza Mkoa wa Dodoma ilipewa shilingi milioni 24 na serikali ili kutengeneza madawati 480 lakini gereza hilo limetengeneza madawati hayo kwa watu binafsi ambapo dawati moja linagharimu 70,000, wakati kila moja lilitakiwa kugharimu shilingi 50,000.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo Jumatano hii wakati alipotembelea gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii mjini hapo.
Alihoji kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma! Hivyo alimtaka Mkuu wa Mkoa, kufuatilia ziada ya Sh 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati inatoka wapi na inakwenda kwa nani.
“Na sasa mmetengeneza madawati kwa shllingi elfu 70 badala ya elfu 50 na madawati mmetengeneza kidogo kuliko yale mengi,mkuu wa mkoa fuatilia hili, na ninazo taarifa hao wanaodaiwa milioni 1.5 wachangie,” aliagiza.
“Fuatilia wanachangia kutoka mifukoni mwao au taasisi, kama taasisi wanapata wapi leo tunashindwa kuwahudumia hawa, wanatoa wapi fedha na taasisi inatoa wapi fedha,” aliendelea kuhoji.
“Sisi tulileta fedha milioni 24 ili tupate madawati 480 kila moja shilingi 50 elfu, kule mtaani nasikia mmepewa kwa shilingi 70, shilingi 20 hii imetoka wapi, inaenda kwa nani? Na kwanini imetumika hivyo? Fuatilia hilo nipate taarifa kamili,” aliagiza.
BY: EMMY MWAIPOPO

0 comments:

Post a Comment