Thursday, October 27, 2016

Lukuvi awageukia wageni na kampuni zinazomiliki ardhi kwa udanganyifu, afuta hati 5


Serikali kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imetoa onyo kwa baadhi ya raia wa kigeni pamoja na kampuni za kigeni zinazomiliki ardhi kinyume cha sheria.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema wizara yake imebaini kuwa wageni hao hutumia nyaraka za kughushi za barua za toleo (ofa) zinazotolewa na Halmshauri za jiji na wilaya, pamoja na hati za kusafiria na vyeti vya kuzaliwa feki ambavyo hutumia kumilikishwa ardhi kinyume cha sheria.
Kuhusu baadhi ya kampuni za kigeni zinazomiliki ardhi kinyume cha sheria, Lukuvi amesema baadhi yao hutumia wazawa kujimilikisha ardhi kinyume cha sheria kutokana kwamba sheria ya ardhi huruhusu kampuni za kigeni zenye wazawa zaidi ya asilimia 50 wanaomiliki hisa kupewa ardhi, na kwamba wageni hao baada ya kumilikishwa ardhi, huwashawishi wazawa kununua hisa zao.
“Tumebaini udanganyifu wa wageni kujimilikisha ardhi kwa mlango wa nyuma,” amesema na kuongeza.
“Natoa onyo kwa wageni wote wanaomiliki ardhi kwa udanganyifu, wajisalimishe. Tutafanya uhakiki tukiwabaini wanaofanya hivyo tutawapeleka mahakamani. Tutafanya hivi ili tuhakikishe kwamba haki ya kumiliki ardhi inatolewa kwa wazawa tu.”
Hata hivyo, Lukuvi amesema wizara yake imefuta hati 5 za raia wa kigeni ambae alifanya udanganyifu na kufanikiwa kupata hati hizo katika mikoa tofauti.
“Nimetoa agizo kwa TAKUKURU kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa ajili ya uchunguzi, na kisha tutamchukulia hatua za kisheria,” amesema.

Source: dewjiblog

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video




0 comments:

Post a Comment