MBUNGE wa Kilombero kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Lijualikali (30) amehukumiwa kwenda jela miezi sita bila faini na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki na uvunjifu wa amani.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo ya wilaya, Timothy Lyon alisema mahakama imewatia hatiani kwa kosa hilo na kwa kuwa mshtakiwa wa kwanza (mbunge) ambaye alikuwa na kesi tatu huko nyuma zilizomtia hatiani, mahakama hiyo imemhukumu kwenda jela miezi sita.
Hakimu Lyon alitaja kesi za nyuma ambazo mbunge huyo alitiwa hatiani na kuhukumiwa kuwa ni namba 338 ya mwaka 2014, namba 220 ya mwaka 2014 na namba 340 ya mwaka 2014.
Alisema mahakama kwa kuona mshtakiwa ni mzoefu na kuona katika kesi zote katiwa hatiani, mahakama imeona mtuhumiwa ana hatia na anapaswa kutumikia kifungo cha miezi sita jela.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Dotto Ngimbwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa (mbunge) akiwa mshtakiwa wa kwanza na mwenzie, Stephano Mgata (35) walitenda kosa hilo Machi mosi mwaka 2016 eneo la Kibaoni katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Ngimbwa alisema washtakiwa hao kwa pamoja, walifanya fujo kinyume na kifungu namba 89 kifungu kidogo cha kwanza B, cha kanuni ya adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Alisema Machi mosi mwaka 2016 saa 4 asubuhi maeneo ya Kibaoni katika maeneo ya ukumbi wa halmashauri, washtakiwa walifanya fujo na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo. Awali, washtakiwa walikana mashtaka na hivyo kufanya kesi kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na upande wa mashtaka ukathibitisha shtaka bila kuacha shaka.
Hata hivyo, mahakama hiyo imeona kwa kuwa mshtakiwa wa pili ni mara ya kwanza, amehukumiwa kifungo cha miezi sita nje, ambapo ndani ya kipindi hicho cha miezi sita hatatakiwa kutenda kosa lolote la jinai.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, hali katika mahakama hiyo ilikuwa tulivu, tofauti na kesi zilizopita, ambapo wanachama wachache walijitokeza licha ya kusambazwa kwa ujumbe ili wajitokeze kwa wingi siku ya hukumu.
Mwandishi wa habari hii alikuta Polisi wachache wakiendelea na shughuli zao na wananchi wakiendelea na shughuli zao na baada ya hukumu kutolewa, mbunge huyo alipelekwa haraka gerezani kutumikia kifungo chake.
Baadhi ya viongozi wa Chadema, walionekana wakiwasiliana na viongozi wa chama hicho makao makuu ya chama, Dar es Salaam ili kulishughulikia suala hilo.
Katiba inasemaje mbunge anapohukumiwa jela?
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 67 (2) (c), mtu hatakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge, ikiwa amehukumiwa zaidi ya miezi sita jela.
Kifungu hicho kinasema; “Mtu hatakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge, ikiwa mtu huyo amehukumiwa na mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita, kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa”.
Source:habarileo
0 comments:
Post a Comment