WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano na Serikali ya China kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu.
Majaliwa aliyasema hayo jana alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, kwa niaba ya Rais John Magufuli kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Alisema ushirikiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria, hivyo ameihakikishia Serikali ya China kwamba utaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.
Aidha, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini zikiwemo za miundombinu, viwanda, kilimo na nishati.
“Tanzania iko tayari kupokea kampuni zaidi za China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini.Tupo tayari kupokea viwanda kati ya 200 hadi 700 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” amesema.
Kwa upande wake, Wang amepongeza utendaji kazi wa Rais Magufuli pamoja na viongozi wengine hususani katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na tayari matunda yameanza kuonekana.
“Serikali ya China kwa sasa iko katika mkakati wa kuhamishia viwanda vyake vingi barani Afrika. Iliamua kuichagua Tanzania kuwa moja katika ya nchi watakayohamishia viwanda hivyo kutokana na kuridhishwa na dhamira inayoonyeshwa na Serikali katika kuleta maendeleo,” alisema Wang.
Wang alisema Serikali China itaendeleza ushirikiano wake na Tanzania kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kujenga uwanja wa ndege na bandari Zanzibar.
Aidha imeahidi kujenga jengo la wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mjini Dodoma ili kuiwezesha wizara hiyo kuhamia mjini humo kama serikali ilivyoelekeza.
Waziri wa wizara hiyo balozi Dk Augustine Mahiga aliyasema hayo jana jijini Dar es salaam baada ya kutembelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi akiwa katika ziara yake ya siku moja ya kikazi.
Dk Mahiga alisema msaada huo wa China ni muendelezo wa ushirikiano ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mao tse tung.
“Hii si mara ya kwanza kwa Waziri huyu kuja nchini ila kwa sasa amekuja kukutana na viongozi wa serikali ya awamu ya tano na amekutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa” alisema.
Alisema miradi mingine itakayotekelezwa ni pamoja na bandari ya Bagamoyo na reli ya Mamlaka ya Reli Tanzania na Tambia (Tazara).
Alisema kwa sasa wanaangalia hali ilivyo na fursa zilizopo pamoja na kutazama maeneo mapya ya kiuchumi na kuyaendeleza.
Wang alisema China inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za kujikomboa hivyo itaendelea kuiunga mkono kuhakikisha inafikia uchumi mzuri.
Source:habarileo
0 comments:
Post a Comment