MASHTAKA 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, yamesababisha Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya kumvua uaskofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Dk Valentine Mokiwa.
Hata hivyo Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezokuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.
Uamuzi wa kumvua uskofu ulichukuliwa juzi na Askofu Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kanisa hilo zilieleza kuwa katika kikao kilichofanyika juzi kanisani Ilala, askofu Chimeledya na ujumbe wake walihudhuria kikao cha halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam akatangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Licha ya uamuzi wa kumvua uaskofu, Dk Chimeledya pia aliagiza waraka unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani, usambazwe kwenye makanisa yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe jana kwenye ibada mbele ya waumini.
“Ni kweli kikao hicho kilifanyika jana, Dk Chimeledya alikuja na katibu mkuu na msajili wa kanisa kwenye kikao, lakini tulishangaa kwamba walikuja na askari polisi kinyume na utaratibu wa kanisa, alisoma maamuzi hayo aliyodai yametolewa na nyumba ya maaskofu,”alisema msemaji wa Dayosisi ya Dar es Salaam Yohana Sanga.
Dk Mokiwa agoma kung’oka
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Padri Jonathan Senyagwa alisema habari hizo sio za kweli na barua ambazo zimesomwa katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam zilisomwa kwa makosa.
“Mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi ni yule aliyemwajiri, na mwajiri wa Dk Mokiwa ni Sinodi ya Dar es Salaam...tutatoa tamko hivi karibuni kuthibitisha kwamba askofu wa jimbo bado hajafukuzwa,” alisema Padri Senyagwa.
Alisema waraka ambao umesambazwa na askofu mkuu wa Tanzania haujapitia kwenye halmashauri ya kudumu ya dayosisi ili kupata baraka zake na wala hauna baraka kutoka kwa sinodi ya dayosisi jambo ambalo linaufanya waraka huo ukose sifa za kutekelezeka.
“Ninachokwambia ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Mokiwa, hatuzitambui barua zilizosomwa katika baadhi ya makanisa,” alisisitiza katibu mkuu huyo wa Dayosisi.
Mgomo huo pia ulithibitishwa na Sanga, ambaye alifafanua kuwa juzi kulifanyika kikao kati ya viongozi wakuu wa kanisa na halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam na kuelezwa na askofu mkuu wa Tanzania Dk Chimeledya hatua ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa jambo ambalo halmashauri iligoma.
“Tulifanyia kikao chetu pale kanisa la Ilala, viongozi wetu wakuu walikuja na polisi wakatusomea huo waraka na kutangaza maamuzi hayo mbele ya halmashauri, lakini maamuzi hayo yaligomewa na wajumbe wa halmashauri ya Dayosisi ya Dar es Salaam,” alisema Sanga.
0 comments:
Post a Comment