Wednesday, October 19, 2016

SERIKALI YATOA BILIONI 80 ZA MIKOPO VYUO VIKUU


SERIKALI imetoa Sh bilioni 80 kwa ajili ya malipo ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaoanza na wanaoendelea na masomo na wameanza kulipwa jana.

Aidha, imewataka wakuu wa vyuo ambao hawajawasilisha matokeo ya wanafunzi wao wanaoendelea na masomo kufanya hivyo haraka ili wakamilishe uchakataji wa mgawo wa mikopo. Katika mwaka huu wa fedha, serikali imetenga Sh bilioni 427 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.



Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akielezea mchakato wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kueleza kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya wanaoanza na wanaoendelea katika robo mwaka.

Manyanya alisema serikali imetoa fedha zinazotakiwa kukamilisha mchakato wa malipo unaofanyika kuanzia jana baada ya kumalizika kwa uchambuzi kulingana na vigezo.

Alisema kwa mujibu wa ulipaji mikopo, inazingatiwa vigezo vya kisheria vya kutoa mikopo kulingana na uhitaji kwa kuangalia anayepewa, kweli ana uhitaji na siyo kwa kila mtu kwani lengo la serikali kusaidia na siyo kuondoa majukumu ya mzazi.

Alisema pia wanaangalia bajeti iliyopo kwa wakati huo, kwani kwa mujibu wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 na matamko ya Rais John Magufuli amedhamiria kuendelea kutoa mikopo kwa wahitaji wote pamoja na kuboresha elimu kwa namna mbalimbali.

Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa sambamba na kutoa mikopo ni ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Mloganzila kwa Sh bilioni 100 pamoja na kukamilisha ukarabati wa vyuo vya ualimu ambapo tayari vyuo 10 vimekamilika.

Alisema pia baada ya Rais kutembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuona adha ya wanafunzi kukabiliwa na kukaa mbali na chuo, Sh bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 20 katika ghorofa tatu zitakazochukua wanafunzi 3,800.

Manyanya alisema pia serikali imelipia ada moja kwa moja vyuoni kwa wanufaika wa mikopo ya Sh bilioni 40 katika vyuo vya serikali na binafsi nchini.



Source: mtembezi

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video




0 comments:

Post a Comment