MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemtaka Gavana wa Benki Kuu (BoT) Benno Ndulu, na Mwendeshaji wa benki ya FBME, Lawrence Mafuru, wafike mahakamani kujieleza jinsi watakavyotekeleza amri iliyoitaka BoT kulipa Sh bilioni 92.
Maofisa hao wanatakiwa kuieleza mahakama watakavyoilipa kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha hizo na kama watashindwa kufanya hivyo, watafungwa jela kama wafungwa wa kesi ya madai.
Utekelezaji wa amri hiyo unatokana na uamuzi wa shauri namba 129 la mwaka 2009, ulioiamuru benki ya FBME kuilipa kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha hizo baada ya kukamata kiwanda chake na kukiuza kwa kampuni ya Five Star Investment ltd.
Uuzwaji wa kiwanda hicho ulitokana na mgogoro wa ulipaji mkopo ambao kampuni ya Coast iliuchukua katika benki hiyo.
BoT inahusishwa kwenye shauri hilo kutokana na kuchukua uendeshaji wa benki ya FBME baada ya benki hiyo kuhusishwa na utakatishaji fedha nchini Cyprus.
Maofisa hao walitakiwa kufika mahakamani hapo Septemba 16 mwaka huu kwa ajili ya kueleza jinsi watakavyotekeleza amri hiyo, lakini hawakufika kwa kuwa wamewasilisha maombi ya kusimamisha shauri hilo ambayo yamepangwa kusikilizwa leo mbele ya Jaji Ama Munisi.
0 comments:
Post a Comment