MATUMIZI ya mafuta ya vyombo vya moto, yameongezeka kwa kasi nchini baada ya serikali kuondoa ada ya mwaka ya vyombo vya moto ambayo watumiaji wa vyombo hivyo walipaswa kulipia kila mwaka.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uingizaji wa Mafuta kwa Pamoja (TBPA), Modestus Lumato alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi na ushindanishwaji wa zabuni za uingizaji wa mafuta kwa matumizi ya mwezi wa tisa mwaka huu.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya mafuta nchini kwa sasa hali iliyosababisha kuongeza meli mbili za mafuta ya ziada kwa ajili ya matumizi ya mwezi wa nane, ili kuhakikisha nchi haikosi mafuta,” alisema Lumato akiihusisha hali hiyo na kufutwa kwa ada ya vyombo vya moto katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18.
Akifafanua alieleza kuwa kwa siku nchi hutumia makadirio ya wastani wa lita milioni 4.7 za dizeli, lita milioni 3.7 za petroli, lita 450,000 za mafuta ya ndege na lita 150,000 za mafuta ya taa.
Awali, Lumato aliongeza kuwa jumla ya zabuni tisa zitawaniwa na kampuni mbalimbali, ambazo zabuni saba ni kwa ajili ya uingizaji wa mafuta kwa matumizi ya mwezi wa tisa na mbili za ziada kwa matumizi ya mwezi wa nane.
“Kwa mwezi wa tisa, tunatarajia kuwa na meli saba, meli tatu kwa ajili ya dizeli tani 360,000, meli tatu za petroli tani 110,000 na meli moja ya mafuta ya ndege na mafuta ya taa,” aliongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBPA.
Katika ushindani wa zabuni hizo, kwa mara ya kwanza kampuni ya Kitanzania, GBP Tanzania Limited ilishinda zabuni ya kuingiza meli moja ya mafuta ya taa na mafuta ya ndege ikizishinda kampuni zingine tatu zilizokuwa zikiwania zabuni hiyo.
Akizungumzia mafanikio hayo, mwakilishi wa GBP Tanzania Limited, Prakash Singh alisema ni jambo la faraja kwao kushinda zabuni hiyo na kuahidi kuwa watafanya vizuri kwa zabuni zijazo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Zabuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja, Ali Ahmed aliipongeza kampuni hiyo kwa kushinda zabuni hiyo, katika ushindani ambao ulihusisha kampuni nne ambazo ni Addax Energy SA, Sahara Energy Resource Limited, Trafigura Pte Limited na Gulf Bulk Petroleum Tanzania Limited.
Wakati huo huo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetoa bei kikomo ya bidhaa za mafuta aina ya petroli kwa mwezi wa nane ambazo zimeendelea kushuka kwa miezi minne kuanzia Aprili, Mei, Julai na Agosti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godwin Samwel, bei zitakazoanza kutumika leo zimeshuka kwa Sh 36 na 44 kwa lita ya petroli na dizeli sawia.
Tofauti ni katika mafuta ya taa, ambapo bei imeongezeka kwa Sh 24 kwa lita, hali iliyosababishwa na kuongezeka kwa gharama ya usafirishaji wa bidhaa ya mafuta katika Mfumo wa Uagizwaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS) Wastani wa matumizi ya mafuta kwa siku ni lita milioni tano, milioni tatu na 100,000 kwa dizeli, petroli na mafuta ya taa sawia.
Kuanzia leo lita moja ya petroli katika Jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh 1,978 kutoka ilivyokuwa mwezi uliopita ya Sh 2,014, wakati lita ya dizeli sasa itauzwa Sh 1,830 kutoka Sh 1,874 na mafuta ya taa yatapanda mpaka Sh 1,830 kutoka Sh 1,806 kwa mwezi uliopita.
Samweli alisema kwa Mkoa wa Tanga, hakutakuwa na mabadiliko kwa petroli na dizeli kwa sababu hakuna mzigo uliopokelewa kupitia Bandari ya Tanga kwa mwezi wa saba 2017.
Hii itafanya bei za bidhaa hizo kwa mkoa huo kubaki kama zilivyokua kwa mwezi wa saba mwaka huu. Taarifa hiyo ilieleza kuwa kampuni za kuuza mafuta ziko huru kuuza bidhaa zao katika bei ya ushindani yenye faida, izingatiwe kwamba bei hizo zisizidi bei elekezi kikomo ya bidhaa iliyokokotolewa kwa kutumia kanuni iliyopitishwa na kutolewa na gazeti la Serikali kupitia GN No.
216 na kuchapishwa Mei 2017. Vituo vya kuuzia mafuta vinakumbushwa kuweka bei za bidhaa za petroli katika mahali panapoonekana, kutofanya hivyo ni kosa kisheria na ina adhabu zake kutoka Ewura.
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment