Rais John Magufuli leo anatarajiwa kupokea ripoti ya Kamati ya Pili ya wachumi na wanasheria, iliyochunguza madini yaliyopo kwenye makontena yenye mchanga wa madini.
Anapokea ripoti hiyo ikiwa ni takribani siku 19 tangu alipokabidhiwa ripoti ya mchanga wa madini, iliyoibua madudu na hata kumlazimu kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari, Rais Magufuli atakabidhiwa ripoti hiyo leo asubuhi Ikulu, Dar es Salaam.
“Tukio hili litarushwa hewani moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya redio, televisheni, mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya Ikulu ambayo niwww.ikulu.go.tz kuanzia saa 3:30 asubuhi,” ilieleza taarifa hiyo. Mei 24, Rais Magufuli alipokea ripoti ya kamati ya kwanza yenye wajumbe wanane waliobobea katika fani za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandishi uchejuaji madini, wakiongozwa na Prof Abdulkarim Mruma.
Kamati hiyo ilichunguza aina na viwango vya madini, yaliyomo kwenye mchanga wa madini uliomo ndani ya makontena, yaliyokuwa yamezuiliwa bandarini na Serikali yasisafirishwe kwenda nje ya nchi. Baada ya kupokea, ripoti hiyo ilionesha mchanga uliokuwa unachunguzwa, ulikuwa na wastani wa kiasi cha thamani kati ya Sh bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani wa chini na Sh trilioni 1.439 kwa kutumia viwango vya juu.
Kutokana na taarifa hiyo, Rais Magufuli aliivunja Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo kutokana na kutosimamia ipasavyo mchakato mzima wa usafirishaji mchanga wenye madini nje ya nchi na hivyo kuisababishia nchi hasara kubwa. Aidha, mbali na kutengua uteuzi wa Waziri Muhongo, alivunja Bodi ya TMAA na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wake. Rais Magufuli pia aliviagiza vyombo vya dola, kuwachunguza na kuwachukulia hatua watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na wengine waliohusika na kushindwa kusimamia vema mchakato mzima wa usafirishaji wa mchanga wenye madini nje ya nchi.
“Nataka niwaambie nchi yetu inachezewa mno, nimekuja kuyaona haya makontena kama yapo, na kweli nimeyaona, sasa utaratibu utakapokamilika nataka Watanzania na dunia nzima ione kilichomo humu ndani kama ni mchanga kweli ama dhahabu,” alisema Rais Magufuli.
Awali, baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku mchanga kusafirishwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mjini Kahama, na kuchukua sampuli ya mchanga wa dhahabu kuupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili aupime na kuona kuna aina ngapi na kiasi gani cha madini kinachopatikana.
Aidha, mbali ya kuunda kamati hizo mbili za wataalamu, Machi 28, mwaka huu Rais Magufuli alimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote inayosababisha nchi kukosa mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba na ulipaji wa kodi.
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment