WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ili taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi, ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha wanalifanyia kazi jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu na muda mwingine kuhoji watoto kuhusu utajiri wanaoupata ghafla.
Majaliwa alisema, “Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa zinakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu.”
Alisema wazazi wanapaswa kujitathmini juu ya malezi ya watoto wao na kujihoji kama wamepata malezi yanayostahili. “Kupitia funzo tulilolipata leo (Jumamosi), tujitathmini kuhusu makuzi ya watoto wetu. Je, watoto wetu wanapata malezi stahiki? Je, tunawalea katika misingi ya kutoa kwa ajili ya Mungu au tunawafundisha wajilimbikizie mali? Je, tunawahoji watoto wetu kuhusu utajiri wanaoupata ghafla? Au tunawapongeza na kufurahia bila kujua wanapata wapi utajiri huo?” Alihoji.
“Nitumie nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya Taifa tunalotaka kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma. Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Mzee Xavery Pinda alifariki Novemba 27, mwaka jana katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kuzikwa kijijini kwake Kibaoni wilayani Mlele, Katavi. Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia Sh milioni 10 ambapo jumla ya Sh milioni 160 zilikusanywa. Kati ya hizo, Sh milioni 111.15 zilikuwa ni ahadi, Sh milioni 38.45 zilikuwa ni fedha taslimu na Sh milioni 10.403 zilikuwa ni thamani ya vifaa vya ujenzi vilivyotolewa.
Naye, Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padre Chesco Msaga alisema kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu kwani hakuna mwanadamu anayeweza kudai kuwa yuko jinsi alivyo kwa sababu ya akili zake. “Hata sisi tunasahau kumshukuru Mungu hasa pale mambo yetu yanapotunyookea. Tunadhani ni kwa akili zetu ndiyo mambo yetu yananyooka.
Tunapaswa tukumbuke kuwa maisha yetu yapo mikononi mwa Mungu, na yeye ndiye anajua njia zetu,” alisema akirejea mfano wa wakoma 10 walioponywa na Bwana Yesu na mmoja tu ndiye alirudi kushukuru. Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema harambee hiyo ilifuatia uamuzi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya wa kuiteua Zuzu iwe parokia.
“Sasa hivi tulikuwa na kigango. Kuteuliwa kuwa parokia maana yake tutakuwa na padre anakaa hapa Zuzu saa 24 na tutakuwa na ibada kila Jumapili, na katikati ya wiki kadri ratiba zitakavyoruhusu.
“Kikubwa tunachopaswa kufanya kufuatia uamuzi huo, ni kuhakikisha kuwa mapadre wana nyumba ya kuishi. Sasa hivi, wa kwetu anakaa Dodoma mjini. Kwa hiyo tuna kazi ya kukarabati kanisa, lakini kwanza tukamilishe ujenzi wa nyumba ya mapadri,” alisema wakati akielezea madhumuni ya harambee hiyo.
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment