WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku na kufuta posho zilizo nje ya utaratibu na zisizotambulika kisheria.
Posho hizo ni za posho za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri za wilaya na manispaa zote nchini. Badala yake, ametaka posho hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo.
Kutokana na agizo hilo, kwa jiji la Dar es Salaam pekee zaidi ya Sh bilioni 130 zilizokuwa zikilipwa kwa halmashauri na manispaa za jiji hilo kwa posho mbalimbali, zitaokolewa na kuingizwa kwenye miradi na shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo ametoa siku tatu kwa watumishi wa umma 10, wanaotakiwa kuripoti katika halmashauri na manispaa mpya ya Kinondoni, kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi. Vinginevyo, watakuwa wamejifukuzisha kwenye utumishi wa umma.
Alisema hayo alipozungumza na watumishi wa Halmashauri na Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam jana katika ziara yake ya siku moja ya kujitambulisha na kukumbushana kuhusu uwajibikaji. Majaliwa aliitaka kila halmashauri hiyo, ifanye tathmini ya mahitaji ya kila kata na kusimamia maendeleo.
Alisema katika halmashauri kumekuwa na matumizi ya fedha nyingi kinyume na taratibu na kanuni. Matumizi hayo huwanufaisha wachache, huku wengine ambao nao waliwajibika wakinyimwa fursa ya kunufaika na wao.
“Utakuta hadi mlinzi anahangaika katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya halmashauri, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje,” alisema.
Alitolea mfano manispaa za Ilala, Temeke na Ubungo kuwa kiasi cha fedha za posho kinacholipwa kwa ajili ya vitafunwa kwa mwaka ni Sh milioni 600, pamoja na posho za mazingira magumu jumla ni Sh milioni 960 kwa kila manispaa.
Kwa upande wa Kinondoni, alisema manispaa hiyo pamoja na vitafunwa ambavyo ni zaidi ya Sh bilioni moja kwa mwaka, pia hulipa posho ya nyuma kwa wakuu wa vitengo kwa mwaka ambayo ni Sh bilioni 2.8.
“Nafuta hizi posho zote ambazo hazitambuliki kisheria, naagiza kuanzia leo malipo haya yapelekwe kwenye shughuli za maendeleo. Naonya Mkurugenzi yeyote nitakayebaini amelipa watu wake posho hizi, amejifukuzisha kazi mwenyewe,” alisisitiza.
Aidha, aliagiza kuwa kiasi cha Sh 800,000 kinachotolewa kwa kila diwani kwa ajili ya kufanya uhamasishaji wa maendeleo kwenye kata yake, kuanzia sasa kisitolewe moja kwa moja kwa diwani, bali kipelekwe kwenye kata na kufuatiliwa namna kinavyotumika.
Pamoja na hayo, Waziri Majaliwa alionya halmashauri zote kuhakikisha kuwa kila fedha inayopelekwa kwenye halmashauri hizo, inatumika kama ilivyokusudiwa. Endapo itabainika kutumika kwa shughuli nyingine, wahusika watachukuliwa hatua.
“Narudia nataka hili lieleweke,kila fedha itakayopelekwa kwa halmashauri itumike kwa lengo lililokusudiwa. Kama ni fedha ya ujenzi wa madarasa iende kwenye ujenzi wa darasa na uendane na thamani ya fedha yenyewe na si vinginevyo,” alisema.
Pamoja na hayo, Kiongozi huyo pia alibainisha kuwa serikali ya awamu ya tano, haitambeba tena mtumishi wa umma yeyote, anayevunja maadili ya utumishi wa umma au anayekosa nidhamu kwa kumhamisha kituo, bali kuanzia sasa mtumishi huyo atafukuzwa kazi.
Aliwataka watumishi wote wa umma nchini, kuwajibika ipasavyo kwa kuhakikisha wanamtumikia vyema mwananchi, ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa.
“Juzi nilipokuwa Longido, nilikuta mtumishi mmoja amesababisha hasara ya takribani Shilingi bilioni 1.2. Baada ya kujua ameharibu, akaomba uhamisho wa kwenda Bahi, tukamzuia, sasa hili ni fundisho, serikali haimbebi tena mtu anayeharibu kazi yake. Hapohapo ulipoharibu ndio tunapomalizana,” alifafanua.
Kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, Waziri Majaliwa alisema serikali imejipanga kuboresha maslahi ya watumishi wote wa umma na ndio maana imeunda timu maalum, kwa ajili ya kuhakiki viwango vya mishahara vinavyotolewa ili kujua kama vinaendana na hali ya maisha.
Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
0 comments:
Post a Comment