KOCHA wa vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba Joseph Omog, amesema kamwe hawahofii mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, URA ya Uganda.
Simba na URA zimepangwa kundi moja la A, katika michuano hiyo inayoendelea kwenye Uwanja wa Amani Visiwani Zanzibar na timu zote zilianza vizuri kwa kupata ushindi ambapo URA, iliifunga KVZ mabao 2-0 na Simba wakaifunga Taifa Jang’ombe 2-1.
Omog raia wa Cameroon, alisema ubora wa kikosi chake ndiyo unamfanya aongee kwa kujiamini na kuwa na uhakika wa kubeba taji hilo mwaka huu.
“Hakuna timu ambayo tunaihofia kwenye mashindano haya kwasababu tuna kikosi bora kuliko timu zote shiriki, na hata hao URA, ambao ndiyo mabingwa watetezi hatuwaogopi tupo tayari kupambana nao na kuwafunga,” alisema Omog.
Kocha huyo alisema amewaangalia kwenye mchezo wao wa ufunguzi dhidi ya KVZ, amegundua kuwa ni timu ya kawaida yenye mapungufu mengi na nimepanga kuwafundisha soka wakati tutakapo kutana kwenye mchezo wa makundi.
Alisema kikosi chake kipo katika wakati mzuri hivisasa na jambo la kuvutia nikwamba wamekuwa wakibadilika kutokana na mpinzani wao anavyocheza kitu cha msingi kwao ikiwa ni ubingwa wa taji hilo ambalo ni muda tangu walitwae.
“Nimeambiwa kuwa mwaka jana walizifunga Simba na Yanga, kama wataingia kwenye mchezo wetu na rekodi hizo watambue wamepotea , Simba hii ipo kwa ajili ya ubingwa kwasababu kila mchezaji anajielewa na anatambua majukumu yake na wao wajiandae kwa kipigo,” alisema Omog.
URA inayofundishwa na kocha Kefa Kisala, ni moja ya timu tishio kwenye michuano ya mwaka huu na inapewa nafasi kub- wa ya kutwaa taji hilo sawa na klabu za Simba, Yanga na Azam ambazo niwageni waalikwa kutoka Tanzania Bara.
Aidha kocha Msaidizi wa timu ya Simba Jackson Mayanja amesema kuwa uushindi wao wa mwanzo umempa faraja na kuona kuwa wameanza mwanzo mzuri wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi katika kuelekea harakati za kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Alisema ushindi wao ni salamu tosha kwa watani wao wa jadi wa timu ya Yanga. Aidha alisema kwamba katika mchezo huo wachezaji wake walicheza vizuri katika kipindi cha kwanza na cha pili walicheza katika kiwango cha chini jambo ambalo alilisemea kuwa ni miongoni mwa makosa ya kimchezo.
“Huu ni mwanzo mzuri na ushindi tulioupata ni salamu kwa wapinzaji wetu, tumekuja kwa ajili ya kupambana ili tuweze kutwaa ubingwa”, alisema.
Hata hivyo alisema kwamba mpira unabadilika lakini watapambana kuhakikisha wanapata ubingwa wa michuano hiyo.
Kwenye mchezo huo uliochezwa wa kundi A, uliochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar, mabao ya Simba yaliyofungwa na Muzamil Yassin na Juma Luizio ambaye anacheza kwa mkopo toka Zesco ya Zambia.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa na kiungo Muzamil Yassin dakika ya 27 kwa mpira uliogonga mwamba kufuatia shuti la beki Method Mwanjali ambalo lilimshinda kipa Ahmed Suleiman.
Juma Luizio akicheza mchezo wake wa pili tangu asajiliwe akafunga kwa shuti la mbali dakika ya 42 baada ya kuwatoka mabeki wawili wa Taifa Jang’ombe.
Beki wa Simba, Novaty Lufunga alijifunga kwa kichwa akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira wa kona ulipigwa na Hassan Bakari wa Taifa Jang’ombe dakika ya 76 na kujipatia bao la kufuta machozi.
Mabingwa watetezi URA iliifunga KVZ mabao 2-0 hivyo Simba inalingana pointi na URA na Taifa iliyoifunga Jang’ombe Boys 1-0 katika mchezo ufunguzi uliochezwa Desemba 30, 2016.
Habari hii imeandikwa na Mohamed Akida, Rahel Pallangyo na Mwajuma Juma, Zanzibar.
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
0 comments:
Post a Comment