Tuesday, January 24, 2017

Kairuki amfuata Mwakyembe Dodoma

AWAMU ya kwanza ya watumishi 87 wa Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inahamia Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia shughuli zote za serikali mkoani humo ifikapo 2020.
Hiyo inakuwa ni wizara ya pili kutangaza hadharani kwamba inahamia Dodoma baada ya mwishoni mwa wiki Wizara ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe kutangaza kuhamia Dodoma kwa viongozi wake wa juu kama ilivyobainishwa katika maelekezo ya kuhamia Makao Makuu ya nchi.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki alisema ofisi hiyo itafunguliwa rasmi mjini Dodoma Januari 30, mwaka huu.
“Nimewaita kuwafahamisha kwamba safari yetu ya kuhamia Dodoma inaanza rasmi sasa... Ahadi ya wizara zote kuhamia Dodoma aliitoa Rais John Magufuli wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika Julai 25, 2016,” alisema Kairuki.
Alisema baadaye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa maelekezo na kuainisha utaratibu wa wizara na taasisi zote za serikali kuhamia makao makuu ya nchi mkoani Dodoma kwa awamu nne.
“Maelekezo hayo yalitaka awamu ya kwanza inayowahusu Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu na baadhi ya watumishi ikamilike ifikapo Februari 28 mwaka huu...Waziri Mkuu alihamia Dodoma Septemba mwaka jana na wizara nyingine zimeendelea na maandalizi ya kutekeleza azma hii ya serikali,” alieleza.
Kutokana na hayo, Kairuki alisema ofisi yake imekamilisha maandalizi ya kuhamia Dodoma, na jana vifaa vya ofisi vya kundi la kwanza la watumishi wa ofisi hiyo vimesafirishwa kwenda Dodoma.
“Kundi hili la kwanza linahusisha uongozi wa juu wa wizara ukiwajumuisha Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, baadhi ya wakurugenzi, wakurugenzi wasaidizi, maofisa waandamizi na watumishi wengine ambao jumla yao ni watumishi 87 wanahamia Dodoma,” alibainisha waziri huyo.
Alisema ofisi yao itakuwa katika Jengo la ‘College of Humanities and Social Sciences’ katika eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kama makao yake ya muda mpaka hapo itakapoelekezwa vinginevyo na anuani ya posta itakuwa ni Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Sanduku la Posta 670, Dodoma.
Kairuki alisema wale wote wanaohitaji kukutana na Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wafike katika ofisi za Dodoma na kufuatia uhamisho huo masuala yote yanayohusu sera na sheria za utumishi wa umma na utawala wa utumishi wa umma kwa ujumla yatatekelezwa katika ofisi ya Dodoma.
Alisema kwa upande wa masuala ya mishahara, uendelezaji, raslimali watu, ukuzaji maadili, anuani za jamii, uchambuzi ushauri na utendaji kazi na huduma ya teknolojia ya habari na mawasiliano yataendelea kushughulikiwa na ofisi ya Dar es Salaam kwa sasa.

Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video



0 comments:

Post a Comment