RAIS John Magufuli ametangaza kuwa serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kununua ndege nyingine nne zikiwemo ndege tatu kubwa, ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja nchini moja kwa moja kutoka nchi zao.
Hatua hiyo inakuja miezi michache tangu serikali yake inunue ndege mbili aina ya Bombardier Q400, ambazo zinafanya kazi katika mikoa mbalimbali nchini zikiwa zimetua nchini kutoka Canada na zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja.
Rais Magufuli ametaja aina ya ndege mpya ambazo serikali itazinunua kuwa ni ndege moja aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika nchini Juni mwakani, ndege mbili aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni 2018.
Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika. Dk Magufuli aliyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani, Jim Deboo ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kununua ndege kubwa kutoka kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Uchukuzi, Dk Leonard Chamriho na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James.
“Sisi hapa tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni mbili kwa mwaka, lakini nchi kama Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu, watalii wakitaka kuja hapa ni lazima waje kwa kuungaunga, wafikie nchi nyingine halafu ndipo wapate moyo wa kuja huku, licha ya kwamba sisi Tanzania ni miongoni mwa nchi tano duniani zenye maeneo mazuri yenye utalii,” alieleza Dk Magufuli.
“Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao,” alisisitiza Rais Magufuli.
Dk Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za Serikali zenye lengo la kuinua utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.
“Tumeleta ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya shilingi laki moja na sitini hadi shilingi laki mbili wakati nauli ilishafika shilingi laki nane na kitu, lakini watu wengine utakuta wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo,” alisisitiza Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini (AfDB), Dk Tonia Kandiero ambaye amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa AfDB Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika ofisi zake zilizopo Afrika Kusini.
Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
0 comments:
Post a Comment