SERIKALI imezipiga stop klabu za Yanga na Simba kuendelea na michakato yao ya kubadili umiliki wake hadi pale yatakapofanyika marekebisho ya katiba zao.
Hayo yalitangazwa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni klabu hizo kongwe ziliazimia kuingia kwenye mabadiliko, Yanga ikikodishwa na mwenyekiti wake Yusuf Manji na Simba ikitaka kuuza hisa asilimia 51 kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.

Kiganja alisema Serikali haikatai mabadiliko ya uendeshaji katika klabu hizo pamoja na nyingine za wanachama, ila inachotaka kwanza kufanyike marekebisho ya katiba zao kwani za sasa haziruhusu mabadiliko hayo.
Alisema kuwa BMT inapenda kuona wahusika wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao, ambapo alisisitiza kuwa kuendelea na michakato hiyo kabla ya kurekebisha katiba zao ni kosa na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Hivi karibuni kumeibuka michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa klabu za wanachama na kuzielekeza katika utaratibu wa hisa na ukodishwaji, vitendo vimesababisha migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani…,” alisema.
Kiganja alisema tayari mezani kwake kuna barua nyingi za wanachama wa Yanga wanaopinga vikali kuendelea kwa mchakato huo wa kubadilisha umiliki.
Source: mtembezi
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
0 comments:
Post a Comment