Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Singida, kimeiomba serikali ya Rais Magufuli kwamba baada ya kumaliza uhaba wa madawati, nguvu zake izielekeze katika kumaliza kulipa madeni ya walimu yakiwemo ya mishahara na yale yasiyokuwa ya mishahara.
Ombi hilo limetolewa jana na mwenyekiti wa CWT mkoa wa Singida, Allani Jumbe, wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waweka hazina wa ngazi ya vitengo walimu wanawake, kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Manyara, Pwani na Dar es Salaam.Mafunzo hayo yanafanyikia ukumbi wa mikutano wa ofisi CWT mkoa wa Singida.
Alisema serikali chini ya uongozi wa rais Dk.Magufuli, imefanya kazi nzuri ya kumaliza uhaba wa madawati katika shule za msingi na sekondari kwa kiwango kikubwa.
“Sasa wanafunzi wetu wamejengewa mazingira mazuri ya kujifunzia ili taaluma iweze kupanda kwa kiwango stahik, ni muda sasa serikali kuelekeza nguvu zake katika kumaliza kulipa madeni ya walimu,” alifafanua Jumbe.
Aidha, alisema tatizo la walimu kupandishwa madaraja na kurekebishiwa mishahara yao kulingana na ngazi zao nalo litafutiwe ufumbuzi wa kudumu.
“Hivi karibuni kumetokea kituko cha aina yake, baadhi ya walimu walipandishwa madaraja, wengine mishahara yao ikarekebishwa na wengine mishahara yao haikurekebishwa kabisa. Baada ya muda mfupi wale ambao mishahara yao ilirekebishwa, marekebisho hayo yakafutwa na kunyang’anywa fedha walizokuwa wamelipwa”,alisema.
Na Nathaniel Limu, Singida
Source: dewjiblog
0 comments:
Post a Comment