Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema ujio wa Mfalme wa Morocco nchini Tanzania ni fursa kubwa ya kibiashara na uwekezaji kwa Tanzania na Morocco ambapo Tanzania imesaini mikataba 21 ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Rais Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Mfalme wa Morocco Mohammed VI ambapo amesema Tanzania ni eneo zuri la uwekezaji pamoja na kuainisha mambo mbalimbali katika mazungumzo yao ikiwemo uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini, utakaosaidia kukuza pato la taifa.
Akitaja baadhi ya makubaliano, Rais Magufuli amekuwa kuwa ni pamoja Mfalme Mohamed VI kuihakikishia nchi kuwa kutakuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka Rabat Morocco hadi Dar es Salaam Tanzania, kutolewa kwa nafasi kwa askari wa Tanzania takribani 150 watakaokwenda kujifunza masuala ya ulinzi na usalama nchini Morocco.
Rais Dkt. John Magufuli amesema amemuomba Mfalme huyo kuijengea Tanzania Msikiti Mkubwa Jijini Dar es salaam na uwanja mkubwa wa mpira mkoani Dodoma jambo ambalo amekubali.
“Nimemuomba Mfalme atujengee uwanja mkubwa wa mpira mkoani Dodoma na Msikiti mkubwa Jijini Dar es salaam jambo ambalo amekubali kitu ambacho kitazidi kuongeza uhusiano wetu kati ya nchi hizi mbili” Amesema Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na mgeni wake Mtukufu Mfalme wa Morocco Mohamed VI pamoja na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es Salaam kushuhudia uwekaji saini Mikataba ya ushirikiano 21 kati ya nchi hizo mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakipigiwa ngoma pamoja na mgeni wake Mtukufu Mfalme wa Morocco Mohamed VI mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment