Monday, September 26, 2016

Timbulo kuwa mwanaume, hadithi ya kuambiwa na Vanessa Mdee ‘Timbulo ndio nani’ iache ipite sasa

Kabla ya kumsikia wiki iliyopita kwenye E-News ya EATV, niliwahi kumsikia tena kwenye kituo hicho hicho akielezea jambo hilo hilo na pia kupitia Siz Kitaa ya Clouds TV. Anadai kuwa aliwahi kumpigia simu Vee Money kumuomba amshirikishe kwenye wimbo wake. Baada ya kujitambulisha yeye ni nani, Timbulo anadai Vee alimuuliza ‘Timbulo ndio nani’ akimaanisha hakuwa akimtambua na hajawahi kumsikia popote.
Timbulo haamini kama Vee Money hamjui, na kwamba alimletea mikausho tu na ilimuuma – in fact inamuuma hadi leo ndio maana ameendelea kuisimulia hadithi hiyo. Anashangaa kuwa iweje Vee aliyekuwa mtangazaji wa redio anashindwa kumfahamu. Niliwahi kumuuliza jambo hilo Vee na aliniambia, “Kusema kweli sikumaanisha kumdharau au kumwonesha kwamba simfahamu Timbulo bali siku zote mtu akiwa anakupigia na namba hauna kitu cha kwanza utauliza ‘haloo haloo, nani mwenzangu’ akasema Timbulo, nikasema ‘Timbulo nani?’ sikumaanisha kwa ubaya lakini kama amechukulia kwa ubaya naomba anisamehe na I hope everything is cool and I wish him all the best.”
Bado nashangaa kwanini Timbulo ameendelea kusimulia jambo hili tena akilipa uzito mkubwa. Kwangu hadithi hii imekwishaanza kunichosha na inaanza kumuonesha kuwa msanii anayetapatapa sasa. Katika muziki, hakuna kitu kinachoweza kumshusha msanii kama tabia ya kulalamika hovyo tena dhidi ya msanii mwenzake. Hiyo inaweza kutafsiriwa kama njia anayotaka kuvuta ‘attention’ katika kipindi ambacho ameikosa.
Mimi hiyo ingenipa hasira ya kufanya kazi nzuri zaidi ili siku moja nisihangaike kujitambulisha tena. Huenda kweli Vanessa alikuwa hamjui na wala hajawahi kumsikia. Timbulo alifanya vizuri zaidi miaka 2011 – 2012 na labda 2013 kidogo, kipindi hicho Vee hakuwa akijulikana kama msanii, zaidi ya VJ wa MTV Base na pia mtangazaji wa Choice FM.



Pamoja na kuwa mtangazaji, aina ya wasanii aliokuwa akikutana nayo hasa kwenye vipindi vyake ni ya tofauti kabisa na Timbulo, hivyo huenda hakuwahi kusikia nyimbo zake. Katika kipindi hiki ambacho Vanessa yupo karibu zaidi na wasanii kwakuwa muziki ndio umekuwa kazi yake, Timbulo hajafanya vizuri na si mtu wa kutengeneza sana headlines. Kwahiyo kumtomjua linaweza kuwa si kosa lake na yumkini watu kibao wengine bado hawamjui.
Lakini, si lazima ujulikane na kila mtu na hicho sio kitu unachotakiwa ukiruhusu ujishushe kwa kujiona bado hujafanikiwa. Kuna wasanii kibao wanajulikana hadi vichochoroni lakini hawana kitu. Kuna wasanii wanaojulikana katika kundi dogo tu la watu lakini muziki wao unawalipa kwa kuwahudumia wao tu. Ni muda wa Timbulo kuipotezea sasa hadithi hiyo kwasababu inaanza kumchoresha na kumuonesha kama mfa maji, ilhali nafahamu uwezo wake wa kuimba ni mkubwa.
Ukiongeza na malalamiko yake mengine dhidi ya Malaika aliyemyeyusha kutokea kwenye video ya wimbo aliomshirikisha, inamfanya aonekane dhaifu. Kimuziki Vee na Malaika wote ni wadogo zake, haimake sense kuendelea kuwalalamikia kwa kitu kile kile. Badala yake ayaache yapite, akaze kutengeneza muziki mzuri zaidi. Kama kila msanii akianza kuyasema hadharani mambo aliyofanyiwa na wasanii wenzake, tungesimuliwwa vioja. Mengine ni vyema kuyakaushia tu. Timbulo kuwa mwanaume, acha yaliyopita yapite.

0 comments:

Post a Comment