Friday, September 8, 2017

Manji aieleza Mahakama kuwa hatambui kuvuliwa udiwani

MFANYABIASHARA Yusuf Manji ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hatambui kuvuliwa udiwani kama ilivyoandikwa kwenye vyombo vya habari.

Manji amesema anatambua kuwa yeye ni Diwani wa Mbagala Kuu na kwamba mahakama imuagize Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) awaambie Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwamba walimkamata na sababu za kutohudhuria vikao kwa miezi miwili ni kwa kuwa hana dhamana.
Ameyasema hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Amesema yeye amechaguliwa na wananchi na kwamba kama wanataka aende kwenye vikao, DPP aombe hati ya kumtoa gerezani ili akaudhurie vikao au wamuandikie barua yenye ajenda na kumbukumbu za vikao ili ajibu akiwa gerezani.
"Nimetumia zaidi ya milioni 70 kwa fedha zangu na sio za halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wangu na nilikuwa nahudhuria vikao kabla sijakamatwa kwa kesi hii nzito.
Kwa kuwa naheshimu mahakama na kesi hii na kwa kuwa naheshimu mahakama hii na ukubwa wa kesi sikuomba dhamana," amesema Manji. Hakimu Shaidi amewataka upande wa mashitaka kufuatilia suala hilo na kwamba maombi yake yamechukuliwa.

Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment