Tuesday, July 18, 2017

Stars tayari kwa safari ya Rwanda

Kikosi cha timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kinatarajiwa kwenda Kigali, Rwanda kesho Jumatano mchana kikitokea Mwanza, Tanzania.
Taifa Stars iliyokuwa jijini Mwanza kwa kambi kabla ya kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Rwanda Jumamosi iliyopita, itapitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere kwenda Rwanda.
Stars itaondoka Mwanza kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania majira ya saa nne asubuhi na kuwasili Dar es Salaam majira ya saa sita mchana kabla ya kuunganisha ndege ya Rwanda majira ya saa nane alasiri kwenda Kigali, Rwanda.
Inakwenda Kigali kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Rwanda maarufu kama Amavubi kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2018). Fainali za CHAN mwakani zitafanyika nchini Kenya.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Mshindi wa jumla katika michezo miwili, atakuwa amesonga mbele hivyo kukutana na Uganda mwezi ujao.
Katika mchezo huo wa marudiano utakachezwa Kigali Rwanda, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga atamkosa beki wake wa kulia, Shomari Kapombe anayesumbuliwa na mguu alioumia katika mchezo kwanza.

source:shaffihdauda
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu

0 comments:

Post a Comment