Tuesday, May 9, 2017

Rais Magufuli kagawa magari mapya Ikulu leo

Ni habari mpya kutokea IKULU Dar es salaam ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa magari mapya matatu aina ya LAND CRUISER kwa Wabunge watatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yao ya Ubunge.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ndio amekabidhi magari hayo ya Wagonjwa kwa niaba ya Rais Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mkoa wa Rukwa Mhe. Ally Keissy, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora Mhe. Munde Tambwe na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Lucy Mayenga.
Balozi Kijazi amesema President Magufuli ametoa magari hayo baada ya kuguswa na kilio cha muda mrefu cha Wabunge hao waliokuwa wakiomba wananchi wao wapatiwe magari ya wagonjwa.
“Mhe. Rais ameamua kuwakabidhi nyinyi haya magari kutokana na vilio vyenu ambavyo amekuwa akivisikia mara kwa mara, Mhe. Keissy umekuwa hata ukitafuta miadi ya kuja kumuona Mhe. Rais kwa suala hili, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyazungumza haya kwa muda mrefu.
“Tunafahamu kila Mbunge katika jimbo lake anahitaji kupata huduma kama hii, na huduma kama hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa hiyo sisi Serikali kila tunapopata uwezo basi tunasaidia pale tunapoweza kufikia kwa wakati ule, tulishatoa magari mengine matatu kama haya Chalinze na vituo vingine vya Morogoro.” Amesema Balozi Kijazi
Balozi Kijazi amewapongeza Wabunge hao kwa kupata magari hayo kwa ajili ya wananchi wao na amewasihi kuhakikisha yanatunzwa vizuri ili yadumu muda mrefu na yawahudumie wananchi wote bila kujali dini, kabila, itikadi zao za kisiasa wala makundi.
Kwa upande wao Mhe. Ally Keissy, Mhe. Munde Tambwe na Mhe. Lucy Mayenga wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuitikia kilio chao cha kuwasaidia wananchi magari ya kubebea wagonjwa, na wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuwapigania Watanzania wote hasa wenye shida na pia kwa juhudi kubwa za kuleta maendeleo.

source:millardayo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment