Monday, April 3, 2017

Mwenge wa Uhuru kunadi uchumi wa viwanda

SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha inafikia uchumi wa kati wa viwanda na kuzalisha bidhaa mbalimbali, ili kuachana na mfumo wa kuagiza kila bidhaa kutoka nje ya nchi.
Hayo yalisemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2017 zilizofanyika mkoani Katavi wilayani Mpanda.
Shamrashamra za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zilihudhuriwa na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Balozi Idd aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alitoa mwito wa kuendelezwa kwa viwanda vilivyopo nchini.
“Tanzania inataka kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Hatua hiyo itafikiwa kama kutakuwa na uchumi wa viwanda. Nchi iwe na uwezo wa kuzalisha bidhaa bora zinazoweza kuhimili ushindani wa soko la kimataifa badala ya kuzalisha malighafi na kuwa soko la bidhaa za viwanda kutoka mataifa mengine,” alisema Balozi Iddi.
Aidha, alieleza kuhusu kupungua kwa vitendo vya rushwa kwa mwaka 2016/2017, na kuipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa jitihada zake.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Takukuru imeendelea kupambana na vitendo vya rushwa kwa kuchunguza, kukamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa vitendo vya rushwa nchini kwa nguvu zote. Jitihada hizo za Takukuru zimefanikiwa kuokoa Sh bilioni 47.18 zilizokuwa zichukuliwa na wala rushwa,” aliongeza.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa mbio hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kufufua viwanda vya kati na viwanda vidogo.
“Ili kufikia malengo hayo Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli imedhamiria kukuza uchumi wa viwanda kwa kufufua viwanda vilivyopo na kuanzisha viwanda vidogo vidogo, vya kati na viwanda vikubwa,” alieleza Jenista na kubainisha kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika mikoa yote 31 nchini na halmashauri 155.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuga alisema kutokana na uzinduzi wa Mwenge mkoani Katavi, kutasaidia kuutangaza mkoa huo.
“Uzinduzi huu wa mbio za Mwenge mwaka 2017, ulisaidia kutangaza mkoa wa Katavi katika njanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na hata kisiasa ndani na nje ya nchi kwa kuwa matangazo haya yanatangazwa moja kwa moja kupitia TBC,” alieleza Muhuga.
Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwa siku 195 katika mikoa yote 31 ya Tanzania ukiwa na kauli isemayo “Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi."
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni Amour Hamad Amour kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati wakimbizaji wengine kitaifa ni Bahati Lugodisha kutoka Geita, Vatima Yunus Hassan kutoka Kusini Pemba, Frederick Ndani wa Singida, Shukrani Islam Mzuri wa Mjini Magharibi na Salome Mwakitalima wa Katavi.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment