Monday, December 5, 2016

Ningemuacha Obrey Chirwa si Mbuyu kumpisha Justine Zulu Yanga

Na Baraka Mbolembole
USAJILI wa kiungo, Mzambia, Justine Zulu katika kikosi cha Yanga SC katika dirisha hili la usajili unafanya idadi ya wachezaji wa kigeni katika timu kufikia nane.
Ili kuendena na kanuni za udhibiti wa wachezaji wa kigeni katika ligi kuu Tanzania Bara, Yanga wanapaswa kupunguza mchezaji mmoja ili wabaki wachezaji 7 wa kigeni kama inavyotakiwa.
Uongozi wa Yanga ulikuwa tayari kuachana na Mnyarwanda mwenye asili ya DR Congo, mlinzi Mbuyu Twite na ulipanga kumuandalia mechi maalum ya kumshukuru ‘kiraka’ huyo mwenye uwezo wa kucheza namba 2, 3, 4, 5 na 6.
Kocha mpya wa timu hiyo raia wa Zambia, George Lwandamina amezuia jambo hilo na amesema anahitaji muda wa kuwatazama wachezaji wake wote-wakiwemo wale wa kigeni ili kuona uwezo wao.
Yanga ina washambuliaji watatu wa kigeni, Mzimbabwe, Donald Ngoma, Mrundi, Amis Tambwe na raia wa Zambia, Obrey Chirwa.
Katika nafasi ya kiungo kuna wachezaji wawili wa kigeni, nahodha msaidizi wa kikosi Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na Mzimbabwe, Thaban Kamusoko na katika nafasi ya ulinzi pia wapo wachezaji wawili kutoka ng’ambo ambao ni Mtogo, Vicent Bossou na Mbuyu.
Kati ya nyota hawa 7, mchezaji mmoja napaswa kuondolewa ili kumpisha kiungo mkabaji, Zulu.
NANI ANAPASWA KUACHWA?
Jukumu hilo analo kocha Lwandamina na timu yake ya ufundi, lakini haituzuii kutoa mawazo yetu.
OBREY CHIRWA
Huyu ni mchezaji ghali zaidi katika ligi kuu Bara msimu huu. Ukiniuliza nani anapaswa kuondolewa, upande wangu ningemuondoa Chirwa.
Licha ya kufanikiwa kufunga magoli matano katika VPL raundi ya kwanza, Chirwa si mfungaji wa kiwango cha juu ambaye anaweza kuibeba Yanga pale anapotakiwa kufanya hivyo.
Mzambia huyo si mshambuliaji bali ni mchezaji mzuri wa nafasi ya kiungo wa pembeni. Ukiwatazama Deus Kaseke, Saimon Msuva, Geofrey Mwashuiya na Juma Mahadhi jinsi wanavyocheza katika nafasi za kiungo wa pembeni ni wazi wachezaji hao wazawa wanaweza kufanya zaidi ya kile ambacho Chirwa anakifanya.
Msuva na Kaseke wamekuwa wakisaidia sana upatikanaji wa magoli katika timu ya Yanga hivyo wawili hawa ndiyo wanachochea kuondolewa kwa Chirwa kwa sababu si mshambuliaji-mfungaji.
NGOMA & TAMBWE
Washambuliaji hawa wawili tayari wameifungia Yanga jumla ya magoli 49 katika VPL tangu walipoanza kucheza Septemba 2015.
Tambwe alifunga magoli 21 wakati alipofanikiwa kushinda tuzo binafsi ya ufungaji bora msimu uliopita. Mrundi huyo amekwishafunga magoli 7 msimu huu. Ngoma yeye alifunga magoli 17 msimu uliopita na mengine manne amefunga msimu huu.
Ushirikiano wao ni mzuri na Yanga yenye Ngoma na Tambwe katika mashambulizi imekuwa ikifunga kwa mipira ya juu na ile ya chini.
Tambwe ni mfungaji asiye na mfano wa magoli ya kichwa, pia amekuwa akijipanga vizuri akiwa ndani ya eneo la hatari.
Ngoma licha ya kuwa ni mmaliziaji hatari pia ni mchezaji mwenye uwezo wa kujitengenezea nafasi, mwenye kasi, nguvu na uwezo wa kukimbia na mpira vizuri.
Kama kocha anahitaji mafanikio katika kazi yake basi wafungaji hawa ni sehemu ya mafanikio yake.
Siwezi kumuacha yeyote kati yao ili kumpisha mchezaji mpya kikosini.
KAMUSOKO & NIYONZIMA
Umeiona Yanga mara ngapi ikicheza vizuri kabla ya wawili hawa kuanza kucheza pamoja? Kitu kilichosaidia sana mafanikio ya mkufunzi aliyepita, Mholland, Hans van der Pluimj ni kutengeneza safu yake ya kiungo na mara baada ya kumsaini, Kamusoko msimu uliopita Niyonzima amekuwa bora zaidi katika kuichezesha timu kwa pasi zake za kutandaza kila upande wa uwanja.
Kamusoko ni mkabaji mzuri lakini pia anauwezo mkubwa sana wa kuipandisha timu kwa kasi. Alifunga magoli yasiyopungua 7 katika michuano yote msimu uliopita kutokana na upigaji wake wa mashuti.
Kila mtu anafahamu uwezo wa Niyonzima ambaye amekuwa mchezaji muhimu wa Yanga tangu Septemba 2011.
Viungo hawa wawili wanapaswa kubaki na kutengeneza ushirikiano na Zulu chaguo la kwanza la Lwandamina.
BOSSOU & MBUYU
Yanga inamuhitaji Zaidi Mtogo, Bossou katika beki yake ya kati, pia inamuhitaji Mbuyu kwa sababu walinzi wengi wa Yanga wana ‘miguu ya glass’ yaani wanaumia mara kwa mara.
Mfano ni Juma Abdul, Kelvin Yondan, Nahodha Nadir Haroub, Oscar Joshua na hata Mwinyi Haji.
Hawa ni wachezaji wanaopata sana majeraha katika kikosi cha Yanga. Uwepo wa Mbuyu huku akiwa na uwqezo wa kucheza nafasi nyingi kwa ufasaha ni sababu ambayo naitazama kwa jicho la tatu na kuona umuhimu wa mlinzi huyu wa kimataifa wa Rwanda.
Yanga inamuhitaji Bossou mlinzi mwenye utulivu na uwezo wa kucheza vyema mbele ya kipa huku akiwapanga na kuwaongoza wenzake.
HITIMISHO
Mimi si kocha wala sina mamlaka ya kusema fulani aachwe na nani asajiliwe ila kwa nilivyoitazama Yanga katika misimu hii miwili ni vyema Lwandamina akaachana na Chirwa kwa sababu timu yake ina washambuliaji wengi wenye viwango bora. Kumuacha Mbuyu ni makosa ambayo watakuja kuyajutia siku za mbele.


Source:shaffih dauda
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video





0 comments:

Post a Comment