Wafanyakazi wa shamba la mipira Kichwele lililopo Wilaya ya Kaskazini “B” wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa utaratibu utakaowapa idhini ya kulihudumia shamba hilo kiuzalishaji baada ya Kampuni iliyopewa jukumu la kuliendesha shamba hilo ya Agro Tec kushindwa kuliendeleza.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma (ZAPSWU) Tawi la Shamba hilo Bibi Kazija Sheha Mohammed alitoa ombi hilo wakati Uongozi wa Chama hicho Taifa ulipofika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufanya mrejesho wa agizo alilowapa mnamo Tarehe 9 Juni mwaka 2016 na kukutana na Wizara ya Fedha kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi wa shamba hilo.
Bibi Kazija ameongeza kuwa wafanyakazi wa shamba la mipira Kichwele kwa sasa wanaendelea kukabiliwa na ukali wa maisha kufuatia Uongozi wa Kampuni ya Agro Tek kusitisha uzalishaji wa mipira uliokwenda sambamba na kulimbikiza madeni ya mishahara ya muda mrefu ya wafanyakazi hao.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amesema Taifa halina nia ya kulikataa ombi la wafanyakazi hao, lakini kinachopaswa kuzingatiwa kwa sasa ni kulifikisha Serikalini ili kuangalia hatua zinazostahiki kuchukuliwa sambamba na kusema Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM ) Imekuwa ikitoa miongozo kwa wananchi kutafuta mbinu za kujiajiri ili kuendesha maisha yao ya kila siku na lazima yasimame katika njia na misingi ya halali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma (ZAPSWU) kwa jitihada unazochukuwa za kufuatilia changamoto zinazowakabili wanachama wao katika taasisi mbali mbali hapa nchini sanjari na kusema kuwa Kampuni ya Agro Tec ilikuwa ikikabiliwa na madeni ya zaidi ya shilingi Milioni 284,839,982/- ikiwa ni pamoja na Mishahara ya wafanyakazi wa mashamba ya Mipira Unguja na Pemba, fedha za likizo pamoja na deni la ZSSF kwa wafanyakazi wake katika kipindi kati ya miezi Mitatu hadi Minane.
Source: mtembezi



0 comments:
Post a Comment