Tuesday, October 4, 2016

Professor J aongea la moyoni

Baada ya msanii mkongwe wa muziki kutoka Morogoro, Afande Sele kumuondoa Professor J katika list ya wasanii wa muziki wa hip hop baada ya kushirikiana na msanii wa Singeli kwenye wimbo ‘Kazi Kazi’, Professor ameamua kufafanua kwanini aliamua mshirikisha msanii wa kisingeli kwenye wimbo hiyo.


Hatua hiyo imekuja baada ya Jumatatu hii, Afande Sele kupitia kipindi cha XXL cha Clouds FM, kudai amekubali alichofanya Professor J kwenye wimbo ‘Kazi Kazi’ lakini amemuondoa msanii huyo katika list ya wasanii wa hip hip baada ya kukiuka miiko ya muziki huyo.
“Professor Jay ni mwanasiasa, mjanja, mwerevu, mwanasiasa anatakiwa awe vile. Jay amesoma alama za nyakati, amefanya kitu ambacho wananchi wake wa Mikumi ambao wamempa kura wanapenda. lakini kisanii kuna watu amewakwaza, kwasababu bahati mbaya hip hop haiishii kwenye muziki tu, hiphop ni utamaduni, kuanzia mavazi, maongezi na kila kitu. Lakini aina ya muziki ambao kafanya ni muziki flani ambao una upotoshaji kwa maadaili ya hiphop, mambo kama kuserebuka, kumwaga razi na vitu kama hivyo. Hicho ndio kimewakwaza watu wa hiphop. Lakini kwangu mimi namchukulia kama mwanasiasa na amefanya kitu ambacho siasa inamtaka kufanya. Na Jay sasa hivi tumtazame kama mwanasiasa na sio mwanahiphop, tukisema ni mwanahiphop tutakuwa tunamkosea sana.” Afande alikiambia kipindi cha XXL cha Clouds FM.

Kauli hiyo ilimvuta Professor J na kuamua kuzungumzia suala hilo ambalo imewagusa wasanii wengi wa muziki wa hip hop nchini.
“Kwanza nimshukuru sana Afande Sele kwa kuzungumza vizuri kwa mapana na maono yake, naheshimu sana maono yake lakini mimi kitu kikubwa ambacho naweza nikawaambia Watanzania ni kwamba sababu kubwa yakufanya wimbo wangu wa sasa ‘Kazi Kazi’ na umefanya vizuri, nikutaka kufanya jambo lingine tofauti. Kwa sababu nimeshafanya kila kitu katika hip hop na watu watakuwa mashahidi. Haya mapinduzi kwenye muziki yamechangiwa sana na Professor Jay, kuwashawishi watu wazima kuona muziki wa hip hop sio uhuni ingawa kuna wahuni wachache wanafanya muziki. Lakini kitu kikubwa ambacho nimejaribu kufanya mimi ni kiongozi, na kiongozi unatakiwa kuonyesha njia kwa wale walio katatamaa. Kama ambavyo nilivyofanya mapinduzi kwenye bongofleva na kuufanya muziki wa bongofleva kuweza kusikika na kuheshimika, nimeona kuna fursa nyingine zipo kwenye muziki wa aina nyingine pia mchango wangu unatakiwa,” Professor J alikiambia kipindi cha Amplifanya cha Clouds FM.
Alifafanua zaidi, “Pamoja kwamba mimi ni kiongozi na ni mbunge wa jimbo la Mikumi lakini pia ni mwanamuziki na pia bado naendelea kuangalia njia ya kufanya mapinduzi katika sehemu nyingine, mfano kwenye muziki wa singeli naona kuna vipaji kabisa, naona kuna watu ambao wanaweza wakafanya kitu ambacho kikasaidia kwenye ajira zao. Kwa hiyo nikaona kama kiongozi sio kitu kibaya kuwatengenezea njia ambayo itawasaidia wao maana Professor J akifanya kitu watu wengi watakiona, ndio maana sasa hivi hata Cholo Mwamba yupo busy na show mikoani, hicho ndo nilichokuwa nataka kukifanya. Lakini bado nimeendelea kubaki pale nilipo, ndio maana nimechana kwenye beat ya Singeli, najua napenda kufanya kitu ambacho mimi nakipenda mwenyewe kwa sababu mimi ni shabiki namba moja wa muziki wangu, lakini najua kuna wengine nitakuwa nimewakwaza. Lakini niwaambie tu wasanii wengine wa hip hop pamoja na mashabiki wa hip hip ambao nitakuwa nimewakwaza, umefika muda sasa wakufanya mambo mengine katika hali ambayo ipo kwenye game, tuache kwenda kwa kukariri kwamba hip hip ni hivi na hivi no, tunatakiwa tufanye kazi katika kiwango chakutosha, kupitia muziki wa singeli ambao unapendwa sana mtaani, nikaona nipenyeze ujumbe wa kuwaambia wafanye kazi, waache kujiuza, waache kuuza madawa, waache kuvuta bangi, wafanye kazi kwa bidii itawasaidia katika maisha yao.,”
Pia rapper huyo amesema ataendelea kufanya muziki wa hip hop katika kiwango cha juu zaidi.

0 comments:

Post a Comment